NA TITO MSELEM-WM
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameahidi kuikutanisha Kampuni ya Lindi Jumbo Limited inayotarajiwa kuanza uchimbaji wa madini ya Kinywe (Graphite) hivi karibuni na taasisi za fedha kwa lengo la kupatiwa mkopo ili ianze uzalishaji wa madini hayo kwa wakati.

Dkt. Kiruswa amesema, Wizara ya Madini imeingia mkataba na mabenki mbalimbali kwa lengo la kutoa mikopo kwa wachimbaji na wafanyabiashara ya madini ambapo ameahidi kuikutanisha Kampuni hiyo na mabenki.
"Mhe. Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi Wizara ya Madini kuwalea na kuwaongoza wachimbaji wa madini ili muweze kufanya shughuli zenu kwa tija, hivyo wiki hii nitazungumza na mabenki ili waone jinsi gani wataweza kuwapatia mkopo muanze uzalishaji wa madini haya muhimu," amesema Dkt. Kiruswa.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa amesema lengo la ziara yake hiyo ni kutaka kujua maendeleo ya Sekta ya Madini katika mkoa wa Lindi na kujua changamoto zinazoikabili sekta hiyo mkoani humo.

Awali, Dkt. Kiruswa alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo kwa lengo la kupata taarifa za shughuli za uchimbaji madini katika mkoa huo.
Aidha, Dkt. Kiruswa ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wachimbaji wa madini kote nchini kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Makarani wa Sensa ili kufanikisha zoezi la kuhesabiwa kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Madini na Taifa kwa ujumla.