Yanga SC yaomboleza kifo cha Dada Hadija, yatoa pole mashabiki waliopata ajali

NA GODFREY NNKO

UONGOZI wa Klabu ya Yanga na Kamati ya Utendaji chini ya Rais Mhandisi Hersi Said umeeleza kupokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya mashabaki wa klabu hiyo.
Ni ajali iliyowapata mashabiki hao wakati wakiwa safarini kuelekea jijini Arusha kuishangilia klabu yao kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC leo Agosti 20, 2022 ikielezea kuwa, katika ajali hiyo shabiki wao maarufu kama Dada Hadija alifariki.

"Uongozi unatoa pole kwa wasafiri wote na familia ya Dada Hadija, pia tunatoa shukrani kwa wote walioshiriki katika kuokoa majeruhi kwenye ajali hiyo, Mola awape ujira mwema.

"Uongozi unaendelea kufuatilia kwa karibu hali za majeruhi hao na utakuwa bega kwa bega kushiriki kila hatua,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, ajali hiyo ambayo ilisababisha kifo na majeruhi kadhaa ilitokea usiku wa Agosti 19, 2022 baada ya gari aina ya Coaster lililobeba mashabiki wa Yanga SC waliokuwa wanatokea jijini Dar es Salaam kuelekea Arusha kupata ajali.

Ni baada ya kugongwa ubavuni na Canter iliyokuwa imebeba mihogo katika eneo la Kiwangwa wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani. Mashabiki hao walitarajiwa leo kushiriki mtanange wa Ligi Kuu ya NBC baina ya Yanga SC na Coastal Union ya jijini Tanga ambao utapigwa katika dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news