Yanga SC,Jackson Group waingia kandarasi kubwa

NA DIRAMAKINI

BINGWA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la Azam kwa msimu wa 2021/2022 na bingwa wa Ngao ya Jamii Tanzania kwa mara ya pili mfululizo, Yanga SC imefanya makubaliano ya ubia wa kimasoko na Kampuni ya Jackson Group kwa kipindi cha miaka miwili.

Jackson Group ni kampuni ya kitanzania inayojihusisha na uwakala wa masoko nchini Tanzania na huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na usimamizi wa haki.

Sambamba na kufanya kazi na wadau wanaojihusisha na udhamini kwenye michezo wakiwa na uzoefu mkubwa wa kufanya kazi na wadhamini wa ndani, Afrika na Ulaya.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam, Rais wa Yanga SC,Mhandisi Hersi Said amesema, “Tunayo furaha kubwa kusaini mkataba huu na kampuni ya Jackson Group.

"Kwa sababu inaenda kufungua milango ya kupata wadhamini na wadau ambao watatusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya klabu yetu, kwani tuna mipango na miradi mingi ambayo inahitaji ushirikiano wa namna hii,”amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jackson Group,Kelvin Twissa alisema, "Ni heshima kubwa kufanya kazi na mabingwa wa kihistoria Young Africans SC, uzoefu wetu wa ndani na wa kimataifa wa kurudushisha thamani ya uwekezaji kwa washirika wetu unaenda kuweka kiwango kipya katika kuwapa thamani wadhamini wetu.

"Tuna fursa nyingi kwa washirika wa ndani na wa kimataifa kuwa sehemu ya mafanikio ya Young Africans SC. Soka nchini Tanzania ina fursa nyingi hata nje ya masoko ya hapa ndani, tuna nia ya kukuza ushirikiano wa vilabu ili kuvutia washirika zaidi na kutoa thamani kwa washirika wetu wa sasa na wanaokuja.

"Young Africans SC walikuwa na msimu wa kipekee msimu uliopita kwa kushinda mataji matatu na imeanza msimu huu mpya kwa kutetea Ngao ya Jamii huku wakionesha kiwango cha hali ya juu ikiwa na kikosi kipya cha msimu huu. Msimu mpya unatoa fursa kwa miradi mingi na ushirikiano ambao utaleta mapinduzi katika masoko ya michezo. katika ukanda huu,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news