Zanzibar yaja na ujenzi mkubwa barabara za mijini, Rais Dkt.Mwinyi asisitiza jambo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuwa wavumilivu na kustahimili changamoto mbalimbali zitakazojitokeza wakati mradi mkubwa wa ujenzi wa Barabara za Mjini utakapoanza.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji wa Saini ya Mradi wa Ujenzi wa Barabara za Juu (Flyover) katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amesaini Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Bi.Khadija Khamis Rajab na kwa upande wa Kampuni ya CCECC kutoka China amesaini Mkurugenzi Mwendeshaji, Bw. Zhang Junle Le, hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu Zanzibar, baada kukamilika hafla ya utiaji saini ya mradi wa ujenzi wa barabara za mjini, unaotarajiwa kutekelezwa na Serikali hivi karibuni kupitia Kampuni ya China Civil Engeneering Construction Cooperation (CCECC) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa China.
Amesema, kuna umuhimu wa wananachi kuwa wastahimilivu wakati mradi huo utakapoanza kutekelezwa kwa kuzingatia kuwa kazi za ujenzi zitaingilia shughuli za wananchi na wakati mwingine kuibua msongamano barabarani.

Kufuatia hali hiyo, Dkt.Mwinyi amevitaka vyombo vya habari nchini kote kuchukua nafasi yao na kuielimisha jamii juu ya kuanza kwa mradi huo mkubwa na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Ameutaka uongozi wa Mkoa Mjini kuanza kuzungumza na wananchi ili waelewe mazingira yatakavyokuwa wakati kazi za ujenzi zikiendelea na kubainisha matumaini yake ya kuwa na Zanzibar mpya pale ujenzi huo utakapokamilika.

Amesema, mkataba wa ujenzi wa barabara hizo unalenga kuubadili Mji wa Zanzibar hivyo akazitaka Idara ya Manispaa kuhakikisha inajianda kuweka sheria ndogondogo kuhusiana na utunzaji wa barabara hususani katika eneo la hifadhi ya barabara.
“Itakuwa haina maana kutumia fedha zote hizo halafu ukute mtu anafanya biashara katika eneo la hifadhi ya barabara,”amesema.

Rais Dkt.Mwinyi alieleza kuwa, hakuna nchi yoyote Duniani ililoweza kupata maendeleo bila ya kuwa na miundombinu bora, hivyo akasema hiyo ndio sababu ilioifanya Serikali kuweka kipaumbele katika suala la uimarishaji wa miundombinu ya barabara Mjini na Vijijini.

Alisema kipaumbele hicho pia kinahusu maeneo mengine, ikiwemo uimarishaji wa Viwanja vya Ndege Unguja na Pemba, Bandari ya Malindi na bandari nyenginezo, uwepo wa umeme wa uhakika pamoja na matumizi ya ICT kwa kuzingatia kuwa uchumi wa kisasa unafanyika Kidigitali.
Rais Dkt.Mwinyi alisema, uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane tayari umekamilisha mikataba ya ujenzi wa barabara za mjini pamoja na ujenzi wa Barabara za Vijijini zenye urefu wa kilomita 200 na akatumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuhakikisha barabara hizo zinakamilika ifikapo mwaka 2025, huku akitaka Wizara Fedha na Mipango kuhakikisha inafanya juhudi za kupata fedha.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt. Khalid Mohamed Salim amesema tukio la utiaji saini ujenzi wa barabara za Mjini ni muendelezo wa juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya kiuchumi hapa nchini.

Amesema, ukuaji wa uchumi unategemea uwepo wa miundombinu bora ya barabara, ambapo hutoa haiba nzuri kwa watumaji na wageni watakaotembelea hapa nchini.

Amesema, barabara nyingi zilizopo Mjini zilijengwa karibu miaka 50 iliyopita, ambapo mbali na kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara zimekuwa zikiharibika hususani wakati wa kipindi cha mvua kubwa na kuilazimu Serikali kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 15 kwa matengenzo.

“Hivyo hatua hii itaondoa matumzii makubwa ya fedha za serikali, itaondoa msongamano, kupunguza ajali barabarani pamoja na kuleta haiba nzuri ya mji wetu,”alisema.

Aliishukuru Serikali kwa juhudi kubwa ilizochukua na kufanikiwa kupata fedha za ujenzi huo, na akatumia fursa hiyo kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt.Mwinyi Talib Haji pamoja na Mwanasheria wa Wizara hiyo kwa kupitia vyema mikataba ya ujenzi huo.

Mapema, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya CCECC, Zhang Junle akiwasilisha ‘Dhana ya Mradi’ huo alisema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara za Mjini utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu, ambapo barabara zenye urefu wa kilomita 100.94 zitajengwa na kuigharimu Serikali kiasi cha Dola za Marekani Milioni 116.1 hadi kukamilika kwake.

Alisema, pamoja na mambo mbalimbali, mradi utahusisha ujenzi wa barabara za juu ‘Flyover’ katika eneo la makutano Amani pamoja na Mwanakwereke.

Alisema wakati wa utekelezaji wa mradi huo wastani wa wananchi 1000 watapata ajira na kusema Kampuni hiyo itakuwa na mashirikiano ya karibu na Serikali pamoja na wananchi. 

Junle alisema Kampuni ya CCECC ni Kampuni kubwa iliyotekeleza miradi mbalimbali mikubwa Barani Afrika na kwingineko duniani, ikihusisha miradi ya ujenzi wa barabara, njia za reli, miundombinu ya usambazaji maji, ujenzi wa daraja pamoja na nyumba za makaazi.

Aidha, alisema hapa Zanzibar ilitekeleza miradi kadhaa ya barabara, ikiwemo barabara ya Bububu-Mahonda- Mkokotoni, Fuoni-Kombeni,Matemwe-Muyuni pamoja na barabara ya Pale-Kiongele, ambapo kwa ujumla zina urefu wa kilomita 54.

Katika hafla hiyo ya utiaji saini ya mkataba wa ujenzi wa Barabara za Mjini, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Khadija Khamis Rajab alitia saini kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,ambapo Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya CCECC, Zhang Junle alitia saini kwa niaba ya kampuni hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news