NA MWANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema chama chake kimejipambanua kuwa ni sauti mbadala kwa wananchi.

Amesema, kwa miaka mingi wananchi walio wengi walikuwa wamekosa sehemu sahihi ya kusemea mambo yao, hivyo sauti mbadala ya wananchi kwasasa ni chama cha ACT Wazalendo.

"Wala hakuna haja ya serikali kukasirika pindi wananchi au sauti mbadala ikieleza kwani kutekeleza matakwa ya wananchi ni sehemu ya uwajibikaji unaohitajika,"amesisitiza Mhe. Othman.

"ACT ipo kwenye serikali kwa sababu tunataka kuirekebisha Zanzibar, na tutahakikisha heshima ya nchi inarudi, kutakuwa na uwajibikaji kwa viongozi na kuwepo chaguzi za haki na ustaarabu," amesisitiza Mhe. Othman.

Amesema Zanzibar ni nchi yenye utajiri mkubwa na iliyokuwa na mamlaka yake kamili, na kama hapatokuwepo sauti mbadala yenye kueleza uhalisia, basi hali ya maisha itazidi kuwa ngumu.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho, Ndugu Ismail Jussa Ladhu, amesema njia pekee ya kuijenga Zanzibar ni siasa za kistaarabu, uwajibikaji wa viongozi wa umma na kuwa na mamlaka yake kamili.

"Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais, jimbo letu lina idadi kubwa ya vijana ambao wapo tayari kupokea maagizo ya chama, na hii ni ishara kubwa kwamba vijana wamekipokea chama na vijana ndio tumaini letu,“alisema Naibu Katibu huyo.
Viongozi mbalimbali kutoka ngazi ya jimbo mkoa na Taifa wakiongozwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Ndg. Salim Bimani, wameambatana na Makamu Mwenyekiti katika katika ziara hio ya ujenzi wa Chama, inayoendelea tena jioni ya leo katika jimbo la Mpendae.