NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, amesema kuwa kushindwa kutumia vyema hazina kubwa iliyopo visiwani hapa ni katiya mambo yanayodhoofisha juhudi za kujenga ustawi bora wa nchi.

Amesema, miongoni mwa hazina hiyo na raslimali muhimu, ambazo zitapelekea majuto, hasa baada ya kuondoka duniani, ni kwamba Zanzibar imebarikiwa kuwa ni Visiwa vya Watu wamoja ambao fungamano la maisha yao pia linatokana na raslimali ya umoja huo.

“Nataka niunganishe pale ambapo amemalizia Katibu wa Sala hii, watu wote wa nchi hii ni wamoja, ambao mila na utamaduni wao, pia unawahamasisha wabaki ni wenye kushikamana na kuishi pamoja, kuendelea kujenga jamii iliyoneemeshwa kama zamani,”ameeleza Alhaj Othman.

Hivyo amewahimiza waumini pamoja na wananchi wote kuwa wasikivu, na wenye kufuata mawaidha mema wanayoyapata katika Misikiti au majukwaa yoyote mema, ili kuhakikisha ustawi bora wa jamii ya watu wamoja.
Akisoma hotuba mbili za sala hiyo,Sheikh Is-haka Vuai Kidawa, amewakumbusha Waislamu, wajibu wa kufuata na kutekeleza mafunzo ya Dini, na kwamba kila mmoja atalipwa kwa mujibu wa mambo mema au mabaya aliyoyatenda katika maisha ya dunia.