Aliyewekewa vikwazo EU,Gervais Ndirakobuca aidhinishwa kuwa Waziri Mkuu nchini Burundi

NA DIRAMAKINI

BUNGE la Jamhuri ya Burundi limemuidhinisha waziri mkuu mpya, ikiwa ni siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuonya kuwa, baadhi ya watu ambao hawakutajwa majina wanapanga kupindua serikali yake.

Katika ujumbe wa Twitter, Bunge lilisema kuwa lilipiga kura kwa kauli moja kumuidhinisha Gervais Ndirakobuca, aliyekuwa Waziri wa Usalama na Masuala ya Ndani kufuatia kuteuliwa kwake na Rais Ndayishimiye.

Mheshimiwa Ndirakobuca ambaye anachukua nafasi ya Alain Guillaume Bunyoni, yuko chini ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya (EU) kwa madai ya kufuta maandamano wakati wa machafuko ya kisiasa mwaka 2015 nchini humo.

Aidha,mwaka 2015, EU iliweka vikwazo vya usafiri na kuzuia mali za Gervais Ndirakobuca na watu wengine watatu
akiwemo Godefroid BIZIMANA, Mathias/Joseph NIYONZIMA (KAZUNGU) na Léonard NGENDAKUMANA baada ya kuwatuhumu kujihusisha na shughuli za kudhoofisha demokrasia kabla ya uchaguzi wa marudio wa mwaka huo wa rais wa wakati huo, Pierre Nkurunziza.

Taifa hilo la Afrika ya Mashariki ambalo kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia kwa mwaka 2020 lina watu milioni 11.89 ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani huku hali ya kisiasa ikiwa haijaimarika kikamilifu.

Katika ujumbe wake wa sauti uliosambaa zaidi nchini Burundi hivi karibuni, Rais Ndayishimiye alisema baadhi ya watu wanajaribu kuiangusha serikali yake na kuwaonya kuwa hawatafanikiwa.

Ndayishimiye ambaye yuko madarakani tangu mwaka 2020 alinukuliwa akisema, “Unadhani jenerali wa jeshi anaweza kutishiwa na wanaosema kwamba wanapanga jaribio la mapinduzi? Nani mtu huyo? Yeyote anayefikiria hilo ajitokeze, kwa nguvu za Mungu, nitamshinda;

Awali Ndayishimiye ambaye ni jenerali wa zamani katika jeshi la Burundi akiwa amezungukwa na watu mashuhuri wa Burundi wakati wa ufunguzi wa hafla ya Mwaka wa Kimahakama wa 2022-2023 iliyofanyika Septemba 2,2022 katika Mkoa wa Gitega alisema, suala la haki ni jambo la msingi kwa watu wote.

Kwa kuzingatia kaulimbiu iliyochaguliwa kwa mwaka huu, "Haki kwa wote, msingi wa maendeleo endelevu", Mkuu huyo wa nchi alisisitiza kuwa hakuna maendeleo bila haki.

Rais Ndayishimiye aliwataka watendaji, watawala,watumishi wa umma na wananchi kila mmoja kutekeleza wajibu wake ili kusimamia haki nchini kwa kurahisisha kazi za mahakimu.

Katika suala hilo, Rais wa Jamhuri hiyo alizitaka mamlaka za utawala kufanya kazi kama baba bora kwa wakati mwingine ya kuchukua nafasi ya mpatanishi pindi unapotokea mgogoro baina ya wananchi wawili au wanafamilia ili kuwaepusha kuchukua hatua za kisheria na hivyo kuwapunguzi mzigo wa kazi mahakimu.

Pia alitaka huduma za umma, hasa utekelezaji wa sheria, kuzuia uhalifu kwa kuimarisha ushirikiano na idadi ya watu ili kesi zinazohusiana na uhalifu zipunguzwe kwa kiasi kikubwa.

"Lazima ujiwekee malengo ya kuondokana na mrundikano wa mahakamani na kuanza kushughulikia majalada mapya,"alidokeza Mkuu huyo wa nchi mbele ya mahakimu kabla ya kueleza nia ya kuona magereza yanaondokana na msongamano ili wafungwa wenye umri wa kuzalisha wachangie katika maendeleo ya nchi.

Mkuu wa Nchi alisifu kazi ya mahakimu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, akitoa wito kwa wananchi wote kuwaunga mkono.

"Kati ya malalamiko yaliyowasilishwa Mahakama Kuu kuhusiana na kesi hizo, asilimia 95 ni hukumu zilizotolewa vizuri,"alisema Mheshimiwa Rais huku akipongeza namna ambavyo mahakimu wengi wa Burundi wanaiheshimu nchi yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news