BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 42

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia... Yeye alisema kulingana na michoro na ramani za majengo tulipaswa kupata mafundi waliobobea katika taaluma ya ujenzi. Yeye alishauri ni vyema tuwaue wachina watano waliokuwa wakisimamia ujenzi wa barabara ya Uvinza kwenda Mpanda kupitia Sumbawanga.
Hawa ndio wangesimamia ujenzi huo na mingine katika GAMBOSHI MPYA wakiwa ni misukule. Mbinja, vifijo na nderemo zililipuka mkutanoni hapo, kila mchawi alionekana kuunga mkono wazo hilo...,Endelea...

Wachawi waliendelea kuchangia mawazo yao juu ya namna ya kukamilisha ujenzi wa majengo hayo ya kambi ya kisasa ya GAMBOSHI MPYA, baada ya kumaliza kikao chao kilifuatiwa na sherehe kubwa. 

Ng'ombe zaidi ya wanane walichinjwa, kulikuwa na idadi kubwa ya mbuzi na kondoo pamoja na maelfu ya kuku. Kulikuwa na vinywaji vya aina mbalimbali, pombe, damu, soda, togwa na vinywaji vingine chungu nzima.

Hapa niseme kidogo, wazo la kuwatumia wafundi katika ujenzi wa GAMBOSHI MPYA pasipo kumwaga damu walimaanisha kuwa. 

Hakukuwa na haja ya kuwafanya mafundi hao kuwa misukule, endapo tungewaua ingepelekea jamii kujua kuwa mafundi hao wamechukuliwa kichawi jambo ambalo lingeleta taharuki. 

Njia iliyokuwa imependekezwa ilikuwa ni nzuri, kwani kupitia njia hii ujenzi ungefanyika usiku. Wakati mafundi wamelala tungewachukua toka majumbani kwao na kuwaleta kwenye eneo la ujenzi. 

Tungewafanyisha kazi mpaka muda ambao tungeona unafaa kuwarudisha. Ujenzi ungeendelea kwa namna hiyo huku tukiwa tumewaua kabisa wachina watano ambao wao wangekuwa misukule kambini hapo kwa ajili ya kusimamia ujenzi wa majengo. 

Hii ni sayansi ambayo huwa tunaitumia sana wachawi katika shughuli zetu, kuna muda unaamka asubuhi umejaa tope miguuni au masikioni tambua ulikwenda kulima. 

Kuna muda unaamka mgongo na shingo vinauma, tambua kuwa ulikwenda kubeba mizigo kwenye shughuli za wachawi. 

Kwa namna moja au nyingine, njia hii iliyoshauriwa na wachawi wengi ilikuwa njia bora katika kufanikisha ujenzi wa GAMBOSHI MPYA. 

The BOMBOM niliungana na wachawi wenzangu kupitia mawazo yao. Baada ya hapo kamati mbalimbali ziliundwa kwa ajili ya namna bora ya kuwapata mafundi na wachina waliokuwa wamekusudiwa. Kikao kilitamatika saa nane za usiku huku kila mmoja akishika njia za kurudi makwake.

Kesho yake muda wa saa tatu usiku tulikwenda stesheni ya treni mji wa Nguruka. Pale tulikuta watu wengi wakiwa kwenye treni ya abiria iliyokuwa njia namba mbili kuelekea Dar es Salaam ikitokea Kigoma. 

Treni hiyo ya abiria isingeweza kwenda kwa kuwa kulikuwa na treni ya mizigo iliyokuwa ikitokea stesheni ya Usinge ikielekea Kigoma. 

Kwa namna hiyo treni ya abiria ilikuwa ikisubiria treni ya mizigo ipite kwanza ndipo ikae njia namba moja. 

Tulipanda kwenye nyungo zetu tukapaa hadi stesheni ya Usinge tukakutana na treni ya mzigo ikiwa njiani. 

Ilikuwa imebeba shehena za vyakula vya kutosha na vitu vingine, kulikuwa na unga wa sembe, ngano, mafuta ya kula nk. 

Lengo letu lilikuwa ni vyakula maana mwaka uliopita mvua hazikuwa nzuri hivyo hatukupata vyakula vya kutosha kambini kwetu.

Wakati treni ikiwa kwenye mwendo tulishuka juu ya mabehewa kisha tukatafuta mabehewa yaliyokuwa na unga na mafuta. 

Bahati nzuri treni hiyo ilikuwa imeunganisha mabehewa kumi na nane, mawili ya nyuma ndiyo yalikuwa yamebeba unga wa sembe na mafuta ya kupikia. 

Tulikwenda kwenye maunganio tukatenganisha wakati treni hiyo ikiwa kwenye mwendo, kwa kuwa ilikuwa usiku dereva hakuweza kujua hilo kwa kuwa tulikuwa tumeshachanganya na dawa. 

Taratibu behewa hizo zilianza kupunguza mwendo kisha zikasimama, tulifungua milango ya mabehewa hayo kisha tukaanza kusomba vyakula hivyo kuvieleka kambini. 

Tulifanya kazi hiyo kwa ustadi wa hali ya juu kwa muda mfupi, kazi ilikamilika kama tulivyokuwa tumeipanga. Baada ya kukamilika kwa kazi hiyo tulirudi kambini kuendelea na shughuli zingine zilizokuwa mbele yetu.

Mambo yote yaliyokuwa yakifanyika kipindi hiki yalikuwa yanahusu utayarishaji wa ujenzi wa GAMBOSHI MPYA. 

Ratiba yetu ilikuwa ikionesha siku iliyokuwa ikifuata ilikuwa ni kwenda kuwachukua wachina. Hata hivyo tulichukua tahadhari ya hali ya juu, mara nyingi watu weupe hujihusisha sana katika masuala ya kichawi. Kwa namna moja au nyingine tulitakiwa kuwa makini sana tusije tukaharibu mipango yetu.

Ilipofika usiku wa saa tano tuliondoka kambini kuelekea eneo walipokuwa wachina, tulitumia usafiri wa ungo kwa kuwa palikuwa mbali kidogo na kambini kwetu. 

Niliambatana na wachawi kumi huku THE BOMBOM nikiwa mkuu wa msafara huo. Tulivuka eneo la Kaguruka, Mlyabibi mji ambao nilizaliwa kisha kutolewa kafara na wazazi wangu. 

Safari yetu ilikuwa nzuri tukiwa kwenye nyungo tatu, hapa niseme kidogo. Ndugu msomaji nyungo ambazo huwa tunatumia wachawi zinatofautiana ukubwa, zipo zinazobeba watu watatu, wanne, watano zingine hata kumi kwa mpigo. 

Usafiri wa ungo haitofautiani na ule wa gari au ndege kwa ukubwa, zipo ndege au gari zinazobeba watu wachache zingine watu wengi. 

Kwa kawaida unapopanda ungo masharti yake ni lazima uwe uchi au umefunga kaniki nyeusi sehemu za siri. 

Ungo huwa na dereva ambaye ndiye huuongoza sehemu za kupita uwapo angani, cha kufurahisha ungo huwa na dashboard ambayo humsaidia dereva kujua kasi aliyonayo.

Mnapoanza safari dereva huamru kila mmoja kusinzia au kufumba macho, hili ni miongoni mwa sharti jingine la kuzingatia mnapokuwa hewani. 

Endapo utakaidi na kufumbua macho utajikuta unadondoka ukiwa hewani, malipo yake ni kifo tu. Mara nyingi nyungo hutua eneo la uwanja wa shule, makanisani, misikitini, juu ya paa nk. 

Baada ya kutua ni dereva mwenye mamlaka ya kuwaambia abiria kufumbua macho baada ya kufika salama safari.

Unaweza kupaa juu sana, karibu au wasitani kutegemea na mapenzi ya dereva. Kwa kawaida madereva wa nyungo huwa hawafumbi macho, abiria wengine ndiyo hupaswa kufumba macho. 

Tuliendelea na safari yetu, tulipokaribia mji wa Musoma pale Malagarasi tulichukua tahadhari sana. Eneo hili lilikuwa ni tishio kwa uhai wetu, hapo ndipo kambi ya Padri Jonasi Chambilacho Muzungu na wenzake ndipo ilipokuwa. 

Hata hivyo tulivuka salama kisha tukaingia mji wa Mpeta, tuliendelea na safari yetu tukiipita miji ya Mabanini, Tandala, Ilunde na hatimaye Uvinza. Kwa kasi tuliyokuwa nayo tulitumia dakika sita kutoka mji wa Majengo kwenda eneo hilo.

Tulivuka mto Luchugi kisha tukatokeza kwenye barabara husika, taratibu tulikwenda kutua kwenye uwanja wa shule ya msingi Nyambutwe. 

Tulishuka kwenye ungo kisha tukaacha nyungo zetu na kufuata kijinjia kinachoelekea kiwanda cha chumvi. 

Kijinjia hicho kilitupeleka mpaka kwenye barabara iliyokuwa ikijengwa. Tuliifuata njia hiyo kwa muda wa dakika kadhaa hatimaye tukafika kwenye kambi ya wachina. 

Ilikuwa kambi kubwa yenye ulinzi wa kila aina, tulitafuta eneo zuri kisha tukaingia ndani yake. Kambi ilikuwa imegawanywa kwenye makundi makundi, sehemu ya kwanza lilikuwa eneo la kupaki gari. Sehemu ya pili ilikuwa ni ofisi, sehemu ya tatu ilikuwa ni eneo la chakula na sehemu ya mwisho pa kulala.

Ndani ya jengo hilo kulikuwa na migomba iliyokuwa imepandwa na kustawi vyema, mara nyingi kambi za wachina huwa kumepandwa migomba. 

Sehemu ya mbele ya kambi hiyo kulikuwa na taa iliyokuwa ikimlika vyema huku bendera za mataifa haya mawili zikipepea. 

Upande wa nyuma wa kambi hiyo kulikuwa na giza, hivyo tukaamua kupitia eneo hilo. Tulikuwa tukitembea kwa tahadhari kubwa kwa kuwahofia wachina hao, kwa mbele yetu tulibahatika kumuona mchina aliyekuwa kabeba mfuko akija upande wetu. Tulikimbia na kujificha karibu na migomba iliyomo kambini humo.

Yule mchina alikuja moja kwa moja eneo tulilokuwa tumejificha kwenye migomba hiyo. Aliangalia huku na huku kuhakikisha kama hakukuwa na mtu aliyekuwa akimuona. 

Alisogea kwenye shina la mgomba mkubwa kisha akabonyeza kidude fulani kilichokuwa kimefichwa eneo hilo. 

Punde si punde pembeni mwa migomba hiyo ardhi ilijifunua akadumbukiza mfuko wake kisha akabonyeza mara ya pili pakajifunga. Mambo haya yalifanyika mbele yetu huku tukishuhudia, aliondoka akatuacha tukiwa bado eneo hilo.

Kwa kuwa tulikuwa tumeshuhudia mambo yote, tuliamua kwenda kubonyeza kitufe hicho kilichokuwa chini ya mgomba. 

Ile ardhi ilijifunua pakawa na shimo kubwa, tulisogea kwenye shimo hilo na kuchungulia ndani. Tulichoshuhudia kilituacha macho kodo, ndani ya shimo hilo kulikuwa na mifupa na mafuvu ya watu mengi. 

Shimo hilo walilitengeneza mahususi kwa lengo la kuficha unyama wao. Kumbe wachina hawa walikuwa wakishiriki kuwaua raia wenzetu! Kumbe wachina hao walikuwa wakishiriki kula nyama za binadamu! Kulikuwa na viunzi vya binadamu vingi. 

Kumbe watu waliokuwa wakipotea wengine walikuwa chakula cha watu hawa! Mpaka kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo ni watu wangapi watapoteza maisha kwa kuliwa?? Ilituuma sana ingawa na sisi tulikuwa ni miongoni mwa watu wanaokula nyama za binadamu.

Tuliamua kuliacha wazi shimo hilo tukawafuata kule walikokuwa wamelala, aliyetangulia kuingia chumbani mwa wachina hao alikuwa ni Jolijo. 

Yeye aliingia ndani kupitia kona ya nyumba, mara baada ya kuingia nilisikia mlio wa risasi paaaaa! Mlio huo ulinishitua kidogo, nikaamua kuingia ndani humo kupitia chini ya ardhi ili kushuhudia nini kilichokuwa kimemsibu Jolijo. 

Tahamaki nilishangaa kumuona Jolijo akiwa sakafuni katambarajika huku bwawa la damu likuwa limemzunguka. Mwili wake uliashiria hakuwa na uhai tena, hisia zangu za awali zilinifanya kuamini kuwa wachina hawa walikuwa wazuri kwenye sayansi ya giza.

Nikazama ardhini kisha nikarudi nje kwa wenzangu kuwaelezea kilichokuwa kimemsibu mwenzetu. Niliwaeleza habari hiyo wakajikuta wanashikwa na hasira za kulipa kisasi, tulichukua dawa ya Wikororo tukaipaka kwenye hirizi ya mzimu kisha tukairusha kwa nguvu hewani. 

Tulisubiri kama dakika tano tukasikia mkolomo ndani ya vyumba hivyo vya wachina, dawa ya Wikororo ni miongoni mwa dawa ambazo huleta usingizi mzito kwa muda mfupi. Tuliamua kufanya hivyo ili wachina hao wasinzie ili tuwashikishe adabu.

Niliingia tena chumbani humo kwa umbo la mbu, lengo langu ilikuwa ni kushuhudia kama mchina huyo alikuwa kasinzia vya kutosha. 

Mkolomo huo ulikuwa ni sahihi, mchina alikuwa kasinzia vya kutosha niliwaita wenzangu wakaingia chumbani humo.

Itaendelea...  

Ukihitaji kisa hiki sehemu ya kwanza hadi ya 40 usisite kutujulisha

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news