NA FRESHA KINASA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Salama Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara, Buhuru Ikungura ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo ambazo zimewezesha miradi mbalimbali kutekelezwa ndani ya kata hiyo.
Amayasema hayo Septemba 12, 2022 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Salama kilichofanyika katika Kijiji cha Salama kati. Ambapo pamoja na mambo mengine amewashukuru wanachama wa chama hicho ngazi ya kata kwa kuwachagua viongozi wapya.
"Namshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kazi nzuri anazozifanya katika kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo. Katika kata yetu ya Salama, tumeona fedha za UVICO-19 zimejenga madarasa vyumba viwili vipya vizuri, barabara zimefunguliwa hii yote ni kuchochea maendeleo ya wananchi katika kata yetu. Tuzidi kumuombea Mheshimiwa Rais na viongozi wote katika taifa letu kwa namna wanavyotekeleza ilani ya CCM,"amesema Buhuru.
Kwa upande wake Emmanuel Maganyara Makoba ambaye ni Diwani wa Kata ya Salama amesema kwamba, ndani ya kipindi cha miaka miwili kata yake imepokea zaidi ya milioni 700 za maendeleo ambapo upande wa TARURA ni shilingi milioni 650, upande wa elimu milioni 145 na fedha za ujenzi wa ofisi ya kata shilingi milioni 45.
Ametoa wito kwa wananchi wa Kata ya Salama na Watanzania kwa ujumla, kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia kwani maendeleo anayoyafanya yana umuhimu mkubwa na faida kwa Watanzania wote.
Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu Wilaya ya Bunda kutoka tawi la Masaba Robinson Wangaso amewaomba wanachama wa chama cha Mapinduzi nfani ya kata hiyo kuwa wamoja kuanzia ngazi za mashina kwani ndio msingi mkubwa wa uimara wa chama hicho.
Wangaso amesema, kuna umuhimu mkubwa kwa wanachama ndani ya chama hicho kuendelea kuweka viongozi wazuri watakaoleta mabadiliko makubwa kwa kuwatumikia wananchi kwa ufanisi hasa ngazi za uwakikishi.
"Tuna haja ya kutimiza wajibu kwa kuwa wamoja na wenye kuthaminiana tuanze kuwa na mkakati ndani ya chama katika kata yetu kwa kuwa na vipaumbele nini kifanyike chenye kuleta manufaa makubwa chini ya Serikali yetu ambayo imejidhatiti kuwaneemesha Watanzania kimaendeleo katika nyanja ya kiuchumi na kijamii."amesema Wangaso.
"Tusiendekeza migogoro kwani hatutafika na Uchaguzi umeshapita tuache makundi, naomba tuanze ngazi za mashina kushikamana hadi Kata kwa kuwa na mpango kazi wa kufanyia kazi kwa muda mwafaka ikiwemo kuongeza idadi ya mashina na matawi, hii itapunguza migogoro na kuimarisha umoja wenye nguvu." amesema Wangaso.