NA SOPHIA FUNDI
MKUU wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Dadi Kolimba amewataka viongozi wa riadha kutumia mbio za Ngorongoro Marathon kutambua vipaji vilivyopo ili kutengeneza timu za kiwilaya na mkoa ambazo zitaweza kwenda kushindana na wenzao katika mashindano ya Kitaifa.
Mkuu wa wilaya ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na wadau wa mchezo wa riadha katika kilele cha maadhimisho ya Ngorongoro Marathon ikiwa ni msimu wa 15 tangu kuanzishwa.
Dadi Kolimba amesema kuwa, mchezo ni muhimu katika maisha ya binadamu, kwani huweza kuepusha magonjwa mbalimbali na ni sehemu ya mazoezi pia ni ajira hivyo wananchi na wadau waendelee kushikamana katika suala zima la michezo ya riadha inayofanyika wilayani hapa.
Kwa upande wake Rais Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Lucas amesema kuwa, mbio za Ngorongoro Marathon zimekuwa ikiwasaidia wanariadha katika maadalizi ya kushiriki mbio za Kimataifa ambapo aliwaomba wadhamini kuendelea kuwekeza kwenye mbio hizo na kuahidi kuwa kwa sasa wana viongozi makini.
Mratibu wa mbio hizo, Meta Petro amewaomba wananchi na wadau kuunga mkono mbio hizo kwani ni kwa ajili ya wana Karatu kuibua vipaji na si kwa ajili yake, kwani riadha ni ajira.
Mbio hizo ambazo zimedhaminiwa na Bonite Botlers Limited,Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zimehitimishwa jana ambapo washindi wa kilomita 21 wanaume na wanawake walipatiwa kiasi cha shilingi milioni moja.