Kamati iliyoundwa na Dkt.Kijazi yabaini vyanzo nane vya migogoro ya ardhi Dar

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya wataalamu kutoka wizarani na Mkoa wa Dar es Salaam iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi imebaini vyanzo nane vinavyochochea migogoro ya ardhi jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Septemba 2, 2022 jijini Dar es Salaam na Dkt.Allan Kijazi wakati akitoa taarifa za matokeo ya ripoti iliyowasilishwa kwake na timu hiyo aliyoiunda Julai 25, mwaka huu.

"Mnamo tarehe 25 Julai, 2022 niliunda Kamati ya Wataalam wa Wizara na Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea na kusikiliza malalamiko ya wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi.

"Kamati hiyo ilijumuisha wataalam kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ili kuongeza uwazi na ufanisi katika zoezi hili. Napenda kuwataarifu kuwa kamati ilianza kutekeleza zoezi hilo kuanzia tarehe 1 Agosti, 2022 hadi tarehe 5 Agosti, 2022.

"Kamati hiyo imekamilisha uchambuzi wa masuala muhimu yaliyojitokeza na inaendelea kuratibu na kusimamia utekeleza wake hasa kwa masuala ambayo vikao vya usuluhishi, uhakiki wa uwandani, ufufuaji wa mipaka, madai ya fidia, upangaji na umilikishaji,"amefafanua Dkt.Kijazi.

Dkt.Kijazi amesema, kamati baada ya kusikiliza, kupitia nyaraka na kufanya uchambuzi wa malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi ilibainisha uwepo wa vyanzo nane vya migogoro na malalamiko ya ardhi katika Mkoa Dar es Salaam.

Dkt.Kijazi amesema kuwa, Kamati ya Wataalam ilipokea malalamiko 391 kutoka kwa wananchi wa halmashauri tano za Mkoa wa Dar es Salaam na hoja tatu kutoka Mkoa wa Pwani katika Wilaya za
Kibaha na Kisarawe.

Amesema kuwa, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jumla ya hoja au malalamiko 41 yaliibuliwa, Kiondoni ni 144, Kigamboni ni 39, Ubungo ni 86, Jiji la Dar es Salaam (Ilala) ni 78 huku kwa upande wa Kibaha na Kisarawe yakiwa malalamiko matatu.

"Kama nilivyoeleza, kamati iliwasikiliza wananchi, ilipokea nyaraka ambazo zilisaidia kufikia uamuzi. Miongoni mwa kazi zilizofanyika ni ukaguzi wa maeneo 36 kati ya 38 yenye changamato za uvamizi, upimaji na kubainisha mipaka.

"Aidha, wananchi 191 wamepewa majibu kwa kuandikiwa barua kuhusu uamuzi au hatua zinazopaswa kuchukuliwa,"amesema Dkt.Kijazi.

Dkt.Kijazi amesema,zoezi la kutatua migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Dar es Salaam ni endelevu ili kuhakikisha maamuzi kuhusu malalamiko yaliyowasilishwa imefikia mwisho.

Aidha, amesema masuala yaliyobakia ambayo ni uhakiki wa uwandani, ufufuaji na urejeshaji wa mipaka, uchambuzi wa madai ya fidia na viwanja mbadala, changamoto zinazotokana na urasimishaji, ukamilishaji wa umilikishaji ardhi, vikao vya usuluhishi yataendelea kufanyiwa kazi hadi ifikapo Septemba 20, 2022.

Kwa upande mwingine, Dkt.Kijazi amesema,kamati imebaini uwepo wa changamoto kwenye maeneo mahususi yenye migogoro ya muda mrefu mathalani Mradi wa Kwembe na Eneo la Kitalu ‘E” Goba Manispaa ya Ubungo.

"Maeneo haya pamoja na maeneo mengine yamewekewa utaratibu maalum wa kuyashughulikia na kuyapatia ufumbuzi kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa,"amesema Dkt.Kijazi.

Kwa mujibu wa Dkt.Kijazi chanzo cha kwanza cha migogoro ni uwepo wa milki pandikizi za ardhi ambapo hoja 13 ziliibuliwa sawa na asilimia 3.3,uvamizi wa maeneo yenye milki za watu wengine ambapo hoja 99 ziliibuliwa sawa na asilimia 25.3.

Vyanzo vingine kwa mujibu wa Dkt.Kijazi ni utapeli ikiwemo kughushi nyaraka ambapo hoja 16 ziliibuliwa sawa na asilimia 4.1, madai ya fidia ambapo hoja 62 ziliibuliwa sawa na asilimia 15.9,uelewa mdogo wa taratibu za ardhi na masuala ya mikataba ambapo hoja 95 ziliibuliwa sawa na asilimia 24.3.

Aidha, Katibu Mkuu Dkt.Kijazi ametaja pia masuala ya mirathi ambapo hoja 12 ziliibuliwa sawa na asilimia 3.1, migogoro iliyotolewa uamuzi na mahakama au mamlaka nyinyinge ambapo hoja 65 ziliibuliwa sawa na asilimia 16.6 na changamoto za urasimishaji ambapo hoja 29 ziliibuliwa sawa na asilimia 7.4.

Wakati huo huo, Dkt.Kijazi amewashukuru wananchi wote waliojitokeza, uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na vyombo vya habari kwa kufanikisha utekelezaji wa zoezi hilo ambalo limekuwa na tija kubwa.

"Aidha, napenda kuushukuru uongozi wa mkoa kwa kuendelea kushughulikia kero na malalamiko ya ardhi za wananchi kwenye maeneo mbalimbali hasa yenye uvamizi wa makundi, hii ni kwa kuwa sote kwa pamoja tunayo dhima kubwa ya kuwahudumia wananchi.

"Baada ya kuhitimisha zoezi hili katika Mkoa wa Dare s Salaam, zoezi kama hili litafanyika kwenye mikoa mingine kwa ratiba ambayo itatolewa hivi karibu ili kupunguza migogoro ya ardhi nchini.

"Nitoe wito kwa wananchi wenye kero na malalamiko kuendeleakuyawasilisha kwenye ofisi zetu za ardhi za mikoa kote nchini ili ziweze kutatuliwa,"amesema Dkt.Kijazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news