NA SOPHIA FUNDI
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha wamelaani tabia ya baadhi ya madaktari kutojaza fomu za PF3 kwa waliofanyiwa vitendo vya ukatili kwa kupoteza ushahidi.

Madiwani hao wameazimia kwa pamoja na kumwagiza mkurugenzi pamoja na timu ya wataalam wa afya wakiwemo ustawi wa jamii kufuatilia kwa karibu madaktari wanaojaza fomu hiyo ya PF3 na kujaza taarifa za uongo kupoteza ushahidi na pale wanapogundulika wachukuliwe hatua za kisheria.
"Haiwezekani kuwanyamazia madaktari hao hata kama ni wa hospitali za binafsi kuendelea kufanya vitendo hivyo , unakuagiza wote hao wako chini yako kwa maana ya halmashauri, hivyo wachukuliwe hatua haraka kukomesha tabia hizo,"alisema Diwani Lucian.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmshauri hiyo, Karia Magaro alisema kuwa halmashauri hiyo imejipanga kutdibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya kata.
Aliwaomba wananchi kuacha tabia ya kulindana na kuficha taarifa za ukatili, bala yake waripoti kwenye kamati za kudhibiti vitendo vya kikatili kwa wanawake na watoto zilizoko kwenye kila kata na pia kwenye dawati la jinsia ili kukomesha vitendo hivyo.
