NA SOPHIA FUNDI
MEYA wa Jiji la Arusha, Maximilian Matle amepongeza Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha kwa kushika nafasi ya tatu kwa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.

Akiwa na wajumbe wa Kamati ya Fedha ya jiji hilo ambao wako wilayani Karatu kwa semina walitembelea halmashauri hiyo kubadilishana uzoefu ambapo alisema kuwa, si jambo rahisi halmashauri kushika nafasi ya tatu Kitaifa, "lakini Karatu mmetisha, hivyo tunawapongeza sana".
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, John Lucian amewashukuru wataalam pamoja na madiwani kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato hadi walipofikia halmashauri kushika nafasi ya tatu Kitaifa.
Amewataka kushirikiana katika kusimamia fedha za ruzuku zilizotolewa na Serikali shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Alisema kuwa, haijawahi tokea serikali inatuma fedha nyingi kwa wakati mmoja, "tena mapema, hivyo hatuna budi kusimamia fedha hizo na zitumike kikamilifu.
"Nina mwaka wa 20 kwenye udiwani sijawahi kuona serikali inatuma fedha za ruzuku mapema hivi na kwa mara moja tunakushukuru sana Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini wana Karatu,asante sana,"alisema Lucian.
Amemwagiza mkurugenzi kuhakikisha fedha hizo zinaingizwa kwenye akaunti za wahusika ndani ya wiki mbili ili ianze kufanya kazi kwa kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu ili mwakani majengo hayo yatumike.
Akifafanua mkurugenzi mtendaji halmashauri hiyo, Karia Magaro alisema kuwa, kiasi hicho cha fedha kitasaidia sana katika ukamilishaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa miradi ya afya,ustawi wa jamii na lishe kiasi cha sh.milioni 800,ujenzi wa madarasa shule kongwe shilingi milioni 180.

Mkurugenzi Mtendaji Karia aliendelea kueleza kuwa, kiasi cha shilingi milioni 50 itatumika katika ujenzi wa bwalo la shule za msingi huku shilingi milioni 200 itatumika kwa ukamilishaji wa nyumba za walimu shule za msingi pamoja na elimu ya awali na msingi kiasi cha shilingi milioni 627.3.
Alisema kuwa, kiasi cha shilingi milioni 120 itatumika katika kukamilika ujenzi wa mabweni shule za sekondari pamoja na ukamilishaji wa maabara shule za sekondari kiasi cha shilingi milioni 180
Halmashauri ya Wilaya ya Karatu wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo kwani ilikuwa hitaji la wana Karatu kwa kukamilika miradi hiyo iliyoelekezwa.