KITU KENYA IMEFANYA

NA LWAGA MWAMBANDE

SEPTEMBA 13, 2022 Dkt.William Ruto aliapishwa rasmi kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya. Mheshimi Ruto alikula kiapo katika uwanja wa Moi Kasarani, kupitia sherehe iliyosimamiwa na msajili wa Idara ya Mahakama Anne Amadi na kushuhudiwa na Jaji Mkuu Martha Koome .

“Mimi, William Samoei Ruto, kwa kutambua kikamilifu wito wa juu ninaochukua kama Rais wa Jamhuri ya Kenya, naapa kwamba nitakuwa mwaminifu wa kweli kwa Jamhuri ya Kenya," aliapa rais mpya Dkt.William Ruto ambaye alikabidhiwa madaraka kwa amani na utulivu, licha ya hapo awali kuonekana kutofautiana na Rais aliyemaliza muda wake, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta.

Hali hiyo, imepeleka picha bora zaidi ndani na nje ya bara la Afrika, ikionesha namna ambavyo nchini Kenya kuna ukomavu wa kidemokrasia na utayari wa kuheshimu maamuzi ya wananchi. Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anakukaribisha upate maarifa kupitia shairi lifuatalo;


>Nchi zinakitamani, kitu Kenya imefanya,
Uchaguzi wa amani, bila mtu kumfinya,
Demokrasi makini, mambo waliyoyafanya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Tuchunguze kwa undani, wenzetu walichofanya,
Tuonayo ya thamani, tuige tuweze fanya,
Yale yasiyo madini, tusije tukayafanya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Machache tumeyaona, tunaweza kuyafanya,
Kuiga si kujiona, hilo mimi nawatonya,
Ili tuweze fanana, chaguzi tukizifanya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Kwa Tume ya Uchaguzi, wako mbali sana Kenya,
Wamepiga kubwa ngazi, kazi inavyozifanya,
Iko huru kwenye kazi, kila mahali yapenya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Iko huru tume yao, si kama tunavyofanya,
Ichaguliwavyo yao, si kama tunavyofanya,
Inaaminika yao, chaguzi zote za Kenya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Uwazi wa uchaguzi, wavutia sana Kenya,
Matangazo waziwazi, vyombo habari vyafanya,
Na hakuna ubaguzi, habari kuminyaminya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Na hili lina mvuto, matangazo wanafanya,
Bomas ule mvuto, habari walitapanya,
Na kwa zote changamoto, mwisho kazi walifanya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Kutangazwa matokeo, tume walivyoyafanya,
Sio kimaendeleo, livyotaka kufanya,
Lakini ni matokeo, ya Katiba yao Kenya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Kingine cha kukiona, kama twaweza kufanya,
Kesi zile tuliona, za uchaguzi wa Kenya,
Urais tuliona, wanapinga watu Kenya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Mahakama ya Upeo, makubwa imeyafanya,
Jambo la maendeleo, kama nasi tukifanya,
Kwamba yote matokeo, yapingwe sawa na Kenya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

>Kenya twawashangilia, uchaguzi wamefanya,
Tena tunafurahia, wazi si kufinyafinya,
Sibaki historia, mema ni vema kufanya,
Kuna kitu kujifunza, jinsi Kenya wamefanya.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news