NA MATHIAS CANA-WEST
KAMATI ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof.Adolf Mkenda kwa kusimamia kwa weledi na ufanisi uratibu wa zoezi la watumishi kuhamia jijini Dodoma kuitikia maelezo ya serikali.
Kauli hiyo ya pongezi imetolewa leo Septemba 8, 2022 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa Ofisi za Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) jijini Dodoma.
Mwenyekiti Nyongo amesema kuwa, wizara hiyo imetii kwa vitendo maelekezo ya serikali ya kuhamia Dodoma ambayo ni maelezo muhimu yaliyotolewa na serikali.
Mhe.Nyongo amesema kuwa kujengwa kwa ofisi na kuhamia jijini Dodoma kutarahisisha wananchi kupata huduma kwa urahisi na ukaribu kwani huduma hiyo ni muhimu kwa usalama wao na usalama wa Taifa kwa ujumla.
“Sisi kama kamati tumeridhika kwa kuja na kuona na tunaahidi tutakuja tena kujionea kazi zinazofanywa pindi jengo litakapoanza kutumika,”amesema Mhe. Nyongo.
Mwenyekiti huyo ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kuwa inawatangazia wananchi kwa kila hali ili waweze kujua kuwa huduma zimerahisishwa na tayari zinapatikana makao makuu ya nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa ziara hiyo ya kamati ya Bunge kuangalia ujenzi wa ofisi za kitaifa za Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) imefikia hatua nzuri za ujenzi na hiyo ni sehemu muhimu katika utekelezaji wa maelekezo ya serikali kuhamia jijini Dodoma.