Dodoma 11 Septemba, 2022.
Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa dhamana ya kusimamia uhifadhi wa maliasili, malikale na maendeleo ya utalii hapa nchini.
Wizara inatekeleza majukumu haya kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni, mipango ya maendeleo na maelekezo mbalimbali ya Serikali.
Katika kipindi cha hivi karibuni Sekta ya utalii hapa nchini imepata mafanikio makubwa kutokana na juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali za kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mikakati ya kukuza vivutio mbalimbali vya utalii vikiwemo hifadhi za wanyamapori, maporomoko ya maji, milima, misitu ya mazingira asilia, utamaduni,fukwe na malikale.
Aidha, kazi kubwa na ya kipekee iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan ya kuvitangaza vivutio vya Utalii vya Tanzania na fursa za uwekezaji kupitia Filamu ya Tanzania The Royal Tour, imekua na matokeo chanya kutokana mwitikio mkubwa wa ujio wa watalii na wawekezaji wanaokuja kuwekeza nchini Tanzania.
Aidha, filamu hiyo imechochea mwamko mkubwa wa shughuli na matukio mbalimbali ya kuhamasisha utalii wa ndani kama vile chakula cha hisani na matamasha ya muziki ambayo yamekuwa yakihusisha uchangishaji wa fedha za kiingilio na wakati mwingine kutoa matangazo ya ushiriki wa Viongozi Wakuu wa Serikali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ili kuwavutia wananchi.
Wizara ya Maliasili na Utalii inautahadharisha umma kuwa makini na matamasha ya aina hiyo na kwamba haihusiki kwa namna yoyote ile katika maandalizi au uchangishaji wa fedha kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali ili kutangaza utalii wa ndani kupitia matamasha yaliyojificha chini ya kivuli cha Filamu ya The Royal Tour.
Imetolewa na;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI