NA DIRAMAKINI
LEO Septemba 17, 2022 viongozi kutoka mikoa ya Kanda ya Kusini ukiwemo wa Mtwara, Lindi na Mtwara wamewashirikisha watanzania na wadau mbalimbali fursa za kiuchumi zilizopo katika mikoa yao.
Sambamba na miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Ni kupitia mjadala wa Kitaifa ulioongozwa na mada juu ya maendeleo na fursa za kiuchumi katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania ambayo ni Mtwara, Lindi na Ruvuma.
Mjadala huo ni mwendelezo wa mijadala ya Kitaifa na Kimataifa ambayo imekuwa ikiratibiwa na Watch Tanzania kwa njia ya Zoom huku ikiwakutanisha wananchi, wadau wa maendeleo, watunga sera, viongozi na wengineo ndani na nje ya nchi.
MHE.KANALI AHMED A. AHMED, MKUU WA MKOA WA MTWARA
"Mkoa wa Mtwara umepata shillingi bilioni 34.5 kwenye sekta ya elimu ambapo elimu bila malipo ni shilingi bilioni 8.735, manejimenti na usimamizi wa mitihani shilingi milioni 3, ukarabati wa vyumba vya madarasa 44 vya sekondari Bilioni 1.350, miradi ya Uviko-19 kwa thamani ya shillingi bilioni 9.460.
"Kuhusu miradi ya Uviko-19 imegharimu shilingi bilioni 4.69, ujenzi wa vituo vya afya kupitia tozo za miamala ya simu ni shilingi Bilioni 6.5 na pia zaidi ya shilingi bilioni 1.3 zimetumika kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati.
"Takwimu zinaonesha Mkoa wa Mtwara ufugaji bado upo chini sana, kwani tuna jumla ya ng'ombe 11,758, mbuzi 67,633, kondoo 74, 285, kuku 9482 na Nguruwe 39,200,"amesema.
MHE. ZAINABU R. TELACK, MKUU WA MKOA WA LINDI
"Shilingi Bilioni 8.3 za tozo zimeweza kujenga vyumba vya madarasa 100, mabweni mawili, na kujenga shule mpya za sekondari 11 na pia tumepata fedha shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa shule maalum za wasichana.
"Tuna changamoto ya kuvua samaki kwenye maji marefu ambako ndio samaki bora hupatikana, hivyo niwaombe wawekezaji kuchangamkia fursa hii kuja na vyombo vya uvuvi vya kisasa kwa ajili ya uvuvi.
"Lindi ina utalii mkubwa wa Bahari ya Hindi, kupitia bahari hii kuna fursa ya ufugaji samaki kwenye vitalu,mabwawa hasa samaki kama kaa, jongo bahari na nyinginezo,"amesema.
MHE. KANALI LABAN THOMAS, MKUU WA MKOA WA RUVUMA
"Mkoa wa Ruvuma una fursa kubwa sana ya kilimo, kwani una hekari milioni nne sawa na asilimia 76 ambazo zinafaa kwa ajili ya kilimo cha mazao ya biashara na chakula na hekari laki nne tu ndio zimetumika, hivyo bado zaidi ya hekari milioni 3.6 ziko wazi.
"Miradi iliyotekelezwa kupitia tozo za miamala ya simu kwa halmashauri Mkoa wa Ruvuma ilikuwa yenye thamani ya shilingi bilioni 5.8125, wilaya ya Mbinga walipata shilingi bilioni 1.5, Halmashauri ya Madaba 275, Halmashauri ya Mbinga milioni 537, Wilaya ya Namtumbo 537, Halmashauri ya Nyasa 537, Halmashauri ya Songea shilingi bilioni 1.
"Kwa mwaka wa fedha wa 2021-2022 kupitia fedha za makusanyo ya tozo, Serikali ilitupatia shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo afya vingine na baadhi kuvifanyia marekebisho, hii yote imewezekana chini ya Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,"amesema.
Tags
Fedha na Uchumi
Fursa za Kiuchumi Tanzania
Habari
Mjadala wa Kitaifa
Uchumi na Biashara
Watch Tanzania