NA FRESHA KINASA
UMOJA wa Machifu mkoani Mara umelipongeza Jeshi la Polisi nchini chini Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania,IJP Camillus Wambura na Chifu Mkuu Hangaya ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa hatua linazoendelea kuchukua kukabiliana na matukio mbalimbali ya kihalifu.
Wameyasema hayo walipokuwa wakizungumza na Waandishi wa Habari septemba 28, 2022 Mjini Musoma mara baada ya kumaliza kikao chao kilichofanyika kujadili hali ya ulinzi na usalama Mkoani Mara Kama viongozi katika jamii.
Chifu Japhet Wanzagi ambaye ni Chifu Wazanaki amesema kuwa, Mkoa wa Mara ulikuwa na matukio mbalimbali ya kihalifu huko nyuma yaliyohusisha mauaji yaliyohusu ushirikina, ramli chonganishi, mauaji ya vikongwe, wezi wa mifugo, na kupiga mishale na hivi karibuni kumezuka matukio makubwa ya kijambazi ambayo yanaathiri mali na maisha ya watu.
"Kufuatia hali hiyo tumeona Jeshi letu la Polisi likipambana na matukio na wahalifu mbalimbali hali iliyorejesha usalama na amani katika mkoa wetu wa Mara. Sisi kama viongozi wa Kimila tunachukua nafasi kulipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua inazozichukua na tunaomba liendelee kufanya operesheni kama hizo katika mikoa yetu Tanzania,"amesema Chifu Wanzagi.
"Tutoe wito kwa watu mbalimbali, kuendelea kudumisha amani ya Mkoa wetu wa Mara na amani ya nchi yetu,"amesema Chifu Wanzagi.
Naye Chief Deus Masanja kutoka Wilaya ya Bunda amewaomba wanasiasa kutochochea migogoro na uvunjifu wa amani kwa uchu wao wa madaraka. Na kwamba jeshi la polisi limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha linaimarisha usalama wa raia na mali zao.
Naye Chief Mwita Matende kutoka Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara amesema chanzo Cha mauaji kipindi Cha nyuma ilikuwa ni migogoro ya ardhi baina ya koo na koo, waganga wa kienyeji kutumia ramli chonganishi, wizi wa mifugo na ahadi za uongo za wanasiasa kuwaahidi wananchi kupanua mipaka ya koo ili wachaguliwe.