NA DIRAMAKINI
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi amesisitiza umuhimu wa jamii kujikita katika kufanya mazoezi kwa kigezo kuwa hujenga afya, kuleta urafiki, upendo na kushajiisha amani.
Mke wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi akijumuika katika mazoezi ya viungo baada ya kumaliza matembezi ya kilomita 5.5 yaliyoazia katika eneo la Legeza mwendo na kumalizika katika viwanja vya mpira Dole Wilaya ya Magharibi “A”Unguja kwa mazoezi ya pamoja ya viungo yalioyofanyika leo, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Majini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana na Waziri wa Habari,Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Tabia Maulid Mwita na kushoto ni Mkuu wa JKU , Kanali Makame Abdalla Daima. (Picha na Ikulu).
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo huko Dole Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja baada ya kukamilisha mazoezi ya viungo, yaliowashirikisha wanamichezo kutoka makundi mbalimbali, ambapo yalitanguliwa na matembezi ya hiari yalioanzia Halmashauri ya Wilaya Magharibi ‘A’ Kianga hadi Viwanja vya Dole.
Akizungumza na wanamichezo hao amesema, mazoezi huleta afya na kufafanua kuwa watu wenye afya huwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi, hivyo akatoa wito kwa jamii kufanya mazoezi kila inapopatikana nafasi na kulifanya jambo hilo kuwa sehemu ya maisha yao.
Amesema kupitia mikusanyiko ya aina hiyo jamii hupata fursa ya kupokea taarifa mbalimbali ikiwemo changamoto zinazowakabili kwa dhamira ya kuzitafutia ufumbuzi.
Mama Mariam alitumia fursa hiyo kuikumbusha jamii juu ya umuhimu wa kuchanja katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19, akibainisha namna watu kadhaa walivyopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Aidha, alielezea umuhimu wa wazazi na walezi katika kusimamia maendeleo ya elimu ya watoto wao pamoja na kufuatilia nyendo zao kwa kigezo kuwa kumekuwa na baadhi ya wanafunzi wanaotoka nyumbani na kuishia njiani wakati wakielekea skuli kwa sababu mbalimbali za utoro.
“Elimu humpa mtu taarifa, maarifa na ustadi pamoja na kusimamia maadili. Elimu ni ufunguo uanaofungua fursa mbambali za kimaisha,”amesema.
Ameeleza kuwa, Taifa linahitaji wataalamu katika fani mbalimbali na kusema elimu ni muhimu katika kufikia malengo hayo.
Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema,wizara hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Mama Mariam Mwinyi kupitia Jumuiya yake ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) katika kuihamasisha jamii kufanya mazoezi.
Mapema, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa aliwashukuru wanamichezo wote walioshiriki mazoezi hayo, ambapo pamoja na amambo mengine alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kijamii zinazokabili wilaya hiyo, akitolea mfano wa suala la utoro shuleni.
Aidha, Mkuu wa wilaya hiyo Suzan Kunambi, aliwashukuru wananchi kwa kuitikia wito wa kushirki katika mazoezi hayo, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono ZMBF na kusisitiza azma ya uongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuwashajiisha.