NA FRESHA KINASA
MKUU wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amesema, Serikali mkoani humo inaunga mkono juhudi zote za maendeleo ya kiuchumi na kijamii zinazofanywa na sekta binafsi mkoani humo.
Amesema, Serikali kazi yake ni kuweka mazingira bora na wezeshi ili wafanyabishara, wajasiramali, wakulima, wafugaji na wachimbaji wa madini waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi ili kuwa na uchumi bora, hivyo mchango wa sekta binafsi una nafasi kubwa katika maendeleo na kwamba serikali itazidi kutoa ushirikiano katika sekta hiyo.
Ameyasema hayo Septemba 11, 2022 wakati akihitimisha maonesho ya kibiashara ya Kimataifa yanayojulikana Kama "Mara Business International Export" ambayo yamefanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara kuanzia Septemba 2 hadi Septemba 11, mwaka huu.
Ambapo wafanyabishara, wajasiramali, wafugaji na taasisi mbalimbali kutoka sekta binafsi na serikalini mikoa mbalimbali wameweza kuonesha bidhaa na kazi zao katika maonesho hayo.
Pia, amewaomba wananchi na wafanyabishara kushirikiana katika kuhakikisha wanapata maeneo kwa wawekezaji ili waje kufanya uwekezaji mkubwa wa kiuchumi.
Boniphace Ndengo ni Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mara ambapo amesema kuwa, maonesho hayo yalikuwa na malengo ya kuutangaza Mkoa wa Mara na fursa zake ziweze kujulikana ili kuwavuta wawekezaji na wafanyabishara kuja kuwekeza ndani ya Mkoa wa Mara.
Pia, kuwaleta pamoja wafanyabishara na wajasiriamali kuonesha bidhaa zao pamoja na kubadilishana mbinu mpya, ujuzi na maarifa ya kukuza biashara sambamba na kuwaleta wadau wote wa sekta binafsi katika kuhakikisha watalii takribani milioni mbili kwa mwaka wanaweza kufika kutalii katika Mkoa huo ambao unahifadhi kubwa ya Serengeti na vivutio mbalimbali vya kitalii.
Ndengo ameiomba serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi katika kuhakikisha sekta binafsi inaendelea kutoa mchango wa kiuchumi mkoani humo, kusaidia mitaji kwa wafanyabishara na wajasiriamali na sera bora ambazo zitaimarisha ufanisi wa kazi zao.
Nao Wananchi Mjini Musoma wamempongeza Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mara, Boniphace kwa namna amavyo amezidi kutoa mchango kuhakikisha sekta binafsi inakuwa mkoani humo katika kuchangia uchumi wa mkoa na wananchi kwa ujumla.