Meena akumbushia jambo wakati wadau wakisubiria ahadi ya Waziri Nape Nnauye

NA MWANDISHI WETU

MJUMBE wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Bw.Neville Meena amesema kuwa,sehemu ya Sheria ya Habari ya Mwaka 1976, kwa miaka 40 ilitoa mwanya kwa mtu mmoja kuamua kufungia chombo cha habari, hata ile iliyotungwa mwaka 2016 imefanya kazi hiyo kwa kuhamisha mamlaka pekee.
Ameyasema hayo leo Septemba 13, 2022 wakati akizungumza katika Kipindi cha Front Page kinachorushwa na Radio +255 Global jijini Dar es Salaam.

‘‘Sheria ya Habari ya Mwaka 1976, imefanya kazi kwa miaka 40, muda wote huo imetoa mwanya kwa mtu mmoja (waziri) kufungia chombo cha habari anapojisikia kufanya hivyo.

‘‘Hata Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipotungwa, imefuata mkondo huo huo wa kutoa mamlaka kwa mtu mmoja kuamua kufungia chombo cha habari ama la ingawa mamlaka hayo amepewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Malelezo. Katika mabadiliko haya, tumeiomba serikali iondoe kipengele hicho,’’amesema Meena.
Amesema, Sheria ya Mwaka 2016 ilianza kulalamikiwa kwa kuwa, haikuondoa mitego iuliyowekwa na sheria ya mwaka 1979, na zaidi imechangia kudumaa kwa vyombo vya habari nchini.

Pia amesema, baada ya wadau wa habari kupiga kelele, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan iliona haja ya kukaa meza moja na wadau wa habari ili kuipatia ufumbuzi.

Meena amesema, hatua za awali alizochukua Rais Samia Suluhu Hassan, ziliongeza ari ya wadau wa habari kushirikiana ili kung’oa vipengele hasi vya sheria ya habari.
‘‘Mwaka jana mwishoni mwa mwezi wa sita, tulikutana na rais (Rais Samia) na akasema, yupo tayari kushughulikia malalamiko yetu.

‘‘Hatua zilianza kuchukuliwa kwa serikali kuleta mapendekezo ya maeneo ya kurekebisha, lakini na sisi tuliongeza yetu ambayo wao walikuwa hawajaweka kwenye mapendekezo yao,"amesema Meena.

Rais Samia

Mei 2,202 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alielekeza Sheria za Habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru vya vyombo vya habari nchini zirekebishwe.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza Sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia.

Rais Samia pia alishauri waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa kuandika mambo mazuri ya kutetea Bara la Afrika huku akiwataka waandishi wa habari kuzitangaza mila na desturi nzuri za Tanzania.

“Tunazo mila na desturi tunapaswa kuzilinda, na nyinyi waandishi wa habari mnatakiwa kuzilinda ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu. Baadhi ya watu wanaposti picha chafu mtandaoni, wanajianika mtandaoni, wengine wanafanya hivyo kwa kutojua madhara ya kufanya hivyo,"alisema Rais Samia.

Meena tena

Aidha,Bw.Meena amefafanua kuwa, wadau wa habari wanachopambana ni kuhakikisha inapatikana sheria rafiki kwa wanahabari na wamailiki wa vyombo vya habari nchini.

Amesema, ingawa kuna baadhi ya sheria zinaozonekana kuwa mbaya hazijatumika, sheria hizo hazipaswi kuwepo kwa kuwa zinatoa mwanya kwa anayetaka kuzitumia kufanya hivyo.

‘‘Kuna sheria zingine zipo na inaelezwa hazijatumika, sheria kama hizo hazipaswi kuwepo maana kuwepo kwake, anaweza kutokea mtu mmoja akazitumia na tukawa hatuna cha kusema.

‘‘Kikubwa katika tasnia ya habari ni kila mmoja atekeleze majukumu yake, serikali ibaki na majukumu yake na wanahabri kama wanataaluma wabaki na majukumu yao,"amesema Meena.

Waziri Nape

Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mheshimiwa Nape Nnauye wakati akihojiwa na BBC alisema kuwa,wanaingia hatua ya pili na wadau wa habari ili pale ambapo hawakukubaliana waweze kujadili kupata mwafaka kwa hatua zaidi.

"Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.

"Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho.

"Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane.

"Kwa hiyo tutakwenda, tutazungumza. Na mimi nina hakika kwamba tutakubaliana na spirit iliyopo ni nzuri, Serikali tupo tayari kuondoa baadhi ya vifungu, kwa sababu hatuna nia mbaya.Lakini pia Jukwaa la Wahariri na wadau wa habari kwa spirit ambayo ninaiona wapo pia tayari kukubaliana baadhi ya mambo. Kwa hiyo twende tukashawishiane,"alifafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

Alifafanua kuwa, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa ujumla wake imelenga kutatua matatizo,"na haya matatizo pande zote mbili tunakubaliana, Serikali na wanahabari,kwa mfano tuna tatizo la kwamba leo mwanahabari akikosea, kinaadhibiwa chombo kizima cha habari, tofauti na ilivyo taaluma nyingine kama udaktari.

"Tunasema tunalitatuaje hilo tatizo,sisi tukasema tumpe leseni huyu mwandishi ili akikosea aadhibiwe binafsi, wenzetu wakasema hili la leseni limekaa vibaya, sisi tukasema sawa, tuwekeeni mezani nini mnadhani kimekaa vizuri, halafu tutashauriana tutafika mahali tutakubaliana.

"Kwa sababu lengo letu ni kutatua changamoto ambazo tunaziona, kwa hiyo Serikali ipo tayari, kikao cha kwanza kimeenda vizuri na nimeridhika,sasa tutakwenda kikao cha pili ambacho nitalazimika kwenda mwenyewe tukae pamoja tuzungumze tujenge hoja, wanawaza nini, tunawaza nini mwishowe tutakubaliana, nchi ni yetu wote,"alisema Mheshimiwa Nape.

"Wajibu wetu wa kwanza ni kusimamia utungaji huu wa sheria ufanyike vizuri na hapa tutakuwa tunajua kwamba marekebisho ya sheria hayafanywi na Serikali. Yanafanywa na Bunge kazi ya Serikali ni kupeleka mapendekezo bungeni halafu yakipitishwa tunatunga sheria.

"Kazi itakayofuata ni kutengeneza kanuni ambazo zitaendena na sheria ambayo imetungwa na mle ndani kuna mambo mengi ya kufanya na mle ndani kuna mchakato ambao hatuusemi sana, mchakato wa kupitia Sera ya Habari.

"Katika nchi yetu ambayo ni msingi mzuri wa kuwa na sheria nzuri kwa hiyo tukaona yote kwa pamoja yaende pamoja, sera inachakatwa na sheria inachakatwa hili la kwanza. La pili hili ni kubwa sana, katika kila utawala uongozi lazima pawepo na political will (utashi wa kisiasa), huo utashi wa kisiasa ndio unaoleta amani na utulivu.

Dhamira ya Serikali

"Nia ya Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri watu watimize wajibu wao, kwa hiyo ikitokea tatizo tunakutana tunakaa mezani hili jambo tunadhani haliko sawa.

"Tunadhani approach hii imesaidia kuwarekebisha wengi, mimi ni muumini wa Baraza Huru la Habari sio tu muumini kwenye hii sheria, mimi ni mwasisi kwa sababu tulipokuwa tunatunga hii sheria ya mwaka 2016 msingi wake ilikuwa kuangalia taaluma nyingine zinajisimamiaje.

"Na hapa lengo letu lilikuwa kupunguza mikono ya Serikali kwenye kusimamia habari, badala yake tuwaachie wanahabari wajisimamie wenyewe yabaki yale mambo ya msingi ya wajibu wa Serikali kulinda usalama wao, watu wake yale ya msingi yatabaki. Lakini haya ya kitaaluma hatuna sababu ya kuyaingilia ya kitaaluma yashughulikiwe na wanahabari wenyewe kwa sababu ndio wenye taaluma yao,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.

"Wanawajibu wa kulinda taaluma yao kama vile wanasheria, madaktari wanalinda heshima ya taaluma yao, wanahabari wana wajibu pia wa kulinda heshima ya taaluma yao,"aliongeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news