NA MWANDISHI WETU
MCHAKATO wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari kamwe hauwezi kuwaacha nje wakuu wa Idara za Uandishi wa Habari, walimu kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya Uandishi wa Habari nchini.
Neville Meena ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wakuu hao wa idara kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya Uandishi wa Habari kuhusu malengo na hatua za Mchakato wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari ulipofika.
"Mchakato huu si wa TEF peke yake, ni muunganiko wa taasisi mbalimbali kwa uchache zikiwemo Twaweza, MISA-TAN, MCT, Jamii Forum.
‘‘Baada ya sheria hii kusainiwa na kuanza kutumika, wadau wa habari tulianza kuipinga ingawa kipindi kilichopita hatukupata ushirikiano kama ilivyo sasa,’’ amesema Meena.
Meena aliwapitisha walimu hao katika baadhi ya vipengele vilivyomo kwenye nakala ya Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria, ikiwemo kipengele cha kutaka kuondolewa kwa utitiri wa vyombo vinavyosimamia tasnia ya habari.
Alieleza kwamba, muundo wa vyombo vilivyoelekezwa na sheria iliyopo, unaweza kuvunjwa na kuunda chombo kimoja ambacho kitakuwa imara na kusimamiwa kisheri kama ilivyo katika taaluma nyingine nchini.
“Sheria inataja kuwepo kwa Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Vyombo vya Habari na pia Mfuko wa waandishi. Kuwa navyombo vyote hivi vinavyofanya kazi ya aina moja, tunasema hapana.
‘‘Hapa tunashauri tuwe na chombo kimoja ambacho kitafanya kazi zote hizo kama ilivyo kwa taaluma za uanasheria, uhasibu, ukandarasi na nyingine ambao hawana utitiri wa vyombo,’’ amesema.
Pia alizungumzia hatua ya sheria kumpa mamlaka makubwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kufungia vyombo vya habari kwa utashi wake.
‘‘Tunasema jambo hili halikukaa vizuri, kumpa mamlaka mtu mmoja kuamua hatma ya kazi za watu sio sawa. Mkurugenzi huyo akifunga chombo maana yake amefunga ajira lakini pia amewanyima haki wasomaji,’’ alisema.
Akizungumzia ukomo wa adhabu ulioweka na sheria hiyo, Meena alisema, sheria ya habari ya mwaka 2016 inaweka adhabu isiyopungua miaka mitatu jela na kwamba, haimpi nafasi hakimu kutoa adhabu chini ya miaka hiyo hata kama kosa ni dogo.
“Tunaamini sio kila kosa linahitaji kifungo cha miaka mitatu. Yapo makosa yanaweza kustahili kifungo cha mwaka mmoja ama miwili lakini pia miezi sita ama onyo.
“Hata kama kosa ni dogo, sheria inamlazimisha hakimu amfunge mwandishi kuanzia miaka mitatu, kwa hakika hili jambo halijakaa sawa. Ndio maana tunasema, vifungu vya namna hii viondolewe,” alisema Meena.