Mgodi wa Williamson Diamond watatua changamoto ya gari kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Shinyanga

NA SAMIR SALUM

CHANGAMOTO ya ukosefu wa gari la zimamoto na uokoaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imepata utatuzi baada kukamilika kwa ukarabati mkubwa wa gari uliofanywa na Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond Ltd uliopo Mwadui wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Katika taarifa yake wakati wa makabidhiano ya gari hilo yaliyofanyika leo Jumanne Septemba 13, 2022 katika mgodi wa Almasi wa Mwadui, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga, Mrakibu George Mrutu ameeleza kuwa, gari hilo lilipata ajali na kupinduka wilayani Kahama ambapo lilikuwa katika majaribio hali iliyopelekea changamoto ya ukosefu wa gari wakati wa majanga ya moto.
Kamanda Mrutu amesema kukamilika kwa ukarabati huo kumeondoa changamoto iliyokuwa ikijitokeza pindi linapotokea tatizo la moto kwa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga na maeneo jirani na kuushukuru uongozi wa mgodi wa Williamson Diamond Ltd huku akiwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za ajali za moto kwa wakati na kwa usahihi ili zitatuliwe.

“Niushukuru sana mgodi wa Williamson Diamond Ltd umeonesha uzalendo kwani wameipunguzia serikali gharama na kuokoa maisha ya watu na mali zao katika Mkoa wa Shinyanga na wamelifanyia marekebisho makubwa hapa linaonekana jipya kabisa kama limetoka Ujerumani, niwaombe wananchi waendelee kutoa taarifa za majanga ya moto kwa wakati,” amesema Kamanda Mrutu.

Kwa upande wake Afisa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Williamson Diamond Ltd, Bernard Mihayo ameeleza kuwa licha ya mgodi huo kuwa na kazi ya kuzalisha Almasi, pia una jukumu la kuihudumia jamii pindi inapokumbana na changamoto hivyo ilijitolea kufanya marekebisho ya gari hilo ikiwa ni sehemu ya kukuza mahusiano na ushirikiano na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Lolote likitokea kwenye jamii sisi lazima tuhusike kutatua changamoto hizo hatuwezi kukaa pembeni, hivi karibuni yametokea matukio ya moto gari hili lingeweza kuzuia hivyo tungependa utunzwaji wa chombo hiki,” ameeleza Mihayo.
Naye Mhandisi Mkuu wa Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond Ltd amesema walipokea maombi kutoka Jeshi la Zima moto na Uokoaji na kutenga muda wa kutengeneza gari hilo kuanzia Julai Mosi hadi Septemba Mosi na umegharimu shilingi Milioni 21.
Gari hilo limekabidhiwa na Afisa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Williamson Diamond Ltd Gerald Mihayo kwa niaba ya Meneja Mkuu wa mgodi huo ambapo limepokelewa na Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoani Shinyanga Mrakibu George Mrutu kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Jeshi hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news