'Mheshimiwa Nape wadau wa habari wanatamani ufanye jambo mwezi huu'

NA MWANDISHI WETU

"Wadau wangependa kuona ahadi ya Mheshimiwa Waziri Nape (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye) ya kupeleka mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari yanafanikiwa kwenye Bunge hili la mwezi Septemba mwaka huu ili mchakato wa mabadiliko hayo ukamilike;

James Marenga ambaye ni Wakili wa Kujitegemea ameyasema hayo leo Septemba 8, 2022 ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Nape kusema kuwa, Serikali inajiandaa kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi za Kimtandao bungeni jijini Dodoma.

Mheshimiwa Nape ameyasema hayo Septemba 7, 2022 wakati akifungua mkutano wa wadau wa mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA ) kwa maana ya Connect to Connect.

Waziri alisema, kwa mara ya kwanza sheria hiyo itasomwa katika mkutano wa Bunge utakaoanza Septemba 13, 2022 jijini Dodoma huku akiwataka wadau watakaokuwa na nafasi za kutoa maoni wafanye hivyo.

Katika kongamano lililowakutanisha wadau wa TEHAMA wakiwemo wa miundombinu kutoka ndani na nje ya Tanzania,Mheshimiwa Waziri Nape aliwataka wadau kutoa maoni huru yatakayopelekwa bungeni na kujadiliwa ili sheria itakayotungwa iwe bora na yenye kulinda taarifa binafsi za Watanzania.

Aidha, Wakili Marenga amesema, wadau wadau wa habari, wangependa kuona Waziri Nape anatimiza ahadi yake ya kuwasilisha mapendekezo ya wadau kuhusu mabadiliko ya sheria za habari katika bunge la mwezi huu.

Amesema, mjadala wa serikali na wadau wa habari ulihusu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kwamba, kuna baadhi ya vipengele tayari wamekubaliana.

“Mjadala wa serikali na wadau ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016, na yaliyojadiliwa ni mapendekezo ya wadau na yale ya serikali, kuna vipengele tulikubalia na vingine bado vipo kwenye mjadala,”amesema Wakili Marenga.

Akizungumzia sheria ya kulinda taarifa binafsi za kimtandao Wakili Marenga amesema, sheria hiyo si ya wadau wa habari pekee bali inahusu watu wote.

“Halafu hii sheria ya data protection (ulinzi wa taarifa binafsi ) sio kwa ajili ya wadau wa habari pekee, ni sheria muhimu kwa watu wote,” amesema Wakili Marenga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news