MSUMBIJI NDUGU ZETU

NA LWAGA MWAMBANDE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan yupo ziarani nchini Msumbiji kwa siku tatu.

Aidha,mbali na mambo mengine ziara hiyo inajikita katika kuimarisha mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii baina ya mataifa hayo mawili ambayo yana historia ndefu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia vikundi vya ngoma za asili za Msumbiji wakati akitoka kuweka shada la maua kwenye eneo la Kumbukumbu ya Mashujaa wa nchi hiyo (Mozambican Heroes’ Square) lililopo Maputo Septemba 21, 2022.(Picha na Ikulu).

Jumatano ya wiki hii mjini Maputo,Mheshimiwa Rais Samia na mwenyeji wake Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji katika mkutano na vyombo vya habari wameonesha utayari wa kuongeza kiwango cha uwekezaji na biashara, ili kuimarisha uchumi na ustawi wa watu wa mataifa hayo mawili.

Rais Samia alisema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Msumbiji kimeshuka kutoka shilingi bilioni 53 hadi kufikia shilingi bilioni 26 katika kipindi cha mwaka huu, hivyo wanahitaji kulifanyia kazi eneo hilo muhimu liweze kuwa na matokeo makubwa.

Amesema, wamekubaliana watumie fursa za kibiashara na uwekezaji hasa katika eneo la kilimo, uvuvi na uchimbaji madini huku Rais Nyusi akisema ziara ya Rais Samia itasaidia kuimarisha uhusiano wao wa kibiashara na kuinua kiwango cha uchumi na uwekezaji.

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande (KiMPAB) anasema kuwa, undugu wetu baina ya Tanzania na Msumbiji ni wa miaka nenda rudi, hivyo muunganiko huo tunapaswa kuutumia kikamilifu ili kuhakikisha unakuwa na matokeo chanya katika nyanja zote kuanzia kiuchumi, kijamii na mengineyo, kupitia shairi lifuatalo,jifunze jambo;


1:Msumbiji ndugu zetu, kwa miaka na miaka,
Kwao huko pia kwetu, kwenda tunafurahika,
Nao wakujua kwetu, sote tunafurahika,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

2:Kwamba Rais Samia, Maputo ameshafika,
Siku kadha kutumia, mengi yaweze jengeka,
Vema sana Tanzania, kumbukumbu kuzishika,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

3:Hata na Rais Nyusi, hapa kwetu lishafika,
Tena lugha yetu nasi, asema achangamka,
Vile kwao kwetu nasi, twaenda nao wafika,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

4:Harakati ukombozi, sote tulishughulika,
Mreno kumpa dozi, hadi huko akatoka,
Ilikuwa kubwa kazi, lakini ilifanyika,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

5:Msumbiji hata kwetu, makazi yalitumika,
Pamoja na mali zetu, mkoloni kupigika,
Pande nyingi nchi yetu, kumbukumbu utadaka,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

6:Mtwara na Bagamoyo, hata Iringa kifika,
Kote walitiwa moyo, vita viweze pigika,
Nyerere pasipo choyo, harakati alishika,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

7:Baada ya kuwa huru, Amani kuimarika,
Nchi zetu ziko huru, kufanya mambo shirika,
Sasa kote kuna nuru, uchumi unajengeka,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

8:Tembea huku na huko, kumbukumbu nyingi daka,
Samora Rais huko, hata hapa asikika,
Tembelea Mbeya huko, uwanja jina ashika,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

9:Jijini Dar es Salaam, nani huyo hajafika,
Au asiyefahamu, mtaa unosifika?
Samora huo fahamu, yule bingwa aenzika,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

10:Sasa kazi moja, Amani kuimarika,
Nchi zetu kwa pamoja, magaidi kuwafyeka,
Ili na sisi pamoja, uchumi weze jengeka,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

11:Rais wetu asante, undugu waimarika,
Rais Nyusi asante, upendo waimarika,
Watoto wetu wapate, histori kuishika,
Vema kutembeleana, kuudumisha undugu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news