NA DIRAMAKINI
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linashiriki Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika karika viwanja vya Bombambili mjini Geita.
Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Bw.Daniel Kure akiwaelezea wananchi kuhusu miradi ya shirika walipotembelea banda la NHC katika maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mjini Geita Mkoa wa Geita.
NHC inashiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kuwafahamisha wananchi juu ya miradi yake mbalimbali inayotekeleza nchini.
Akizungumza na baadhi ya wananchi waliofika katika banda la NHC, Afisa Mauzo na Masoko Mwandamizi, Bw. Daniel Kure amewajulisha wananchi hao juu ya uuzaji wa nyumba za makazi zilizopo Iyumbu na mradi wa nyumba za makazi ujulikanao kama Samia Housing Scheme (SHC) utakaojengwa katika eneo la Tanganyika Packers Kawe jijini Dar es Salaam.

Bw.Kure ameongeza kuwa, katika mradi huo wa Iyumbu pia kuna nyumba za vyumba vitatu zenye ukubwa wa square mita 120 ambazo zinauzwa kwa bei ya shilingi milioni 83 hadi shilingi milioni 87. Ambako huko nyumba zimegawanyika katika ukubwa tofauti zikiwemo za ukubwa wa square mita 75, 100 na 120.

"SHS ni mradi mkubwa upakaokuwa na nyumba za aina tatu zikiwemo za ukubwa wa square mita 89.5 vyumba vitatu, square mita 67.7 vyumba viwili na square mita 21.2 chumba kimoja na vyumba vyote hivi vina master bedroom,"amesema Bw.Kure.
Miongoni mwa wateja, Bi.Anna Mwandesya akizungumza na Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Bw.Daniel Kure alipotembelea banda la NHC katika maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mjini Geita Mkoa wa Geita.
Aidha, baada ya Bw.Kure kutoa maelezo hayo,mmoja wa wananchi waliofika kwenye banda la NHC, Bi. Anna Mwandesya alionesha kufurahishwa na uanzishwaji wa mradi wa Samia Housing Scheme (SHC) na kusema kuwa utakuwa mkombozi kwa wananchi kwa kuwa unatoa fursa ya kila mwananchi mwenye uwezo kupata nyumba hizo.
"Kwanza niwapongeze NHC kwa kazi kubwa mnayoifanya, lakini niwaombe mtujengee na sisi hapa jengo kubwa la biashara kama ambavyo tunasikia kwa mikoa mingine mlivyojenga ili nasi mbali ya kunufaika na nyumba mlizozijenga Bombambili basi nasi wafanyabiashara tupate jengo kubwa la biashara kwa kuwa kodi zenu ni rafiki tofauti na tupakopanga kwa watu binafsi,"amesema Mwandesya.

Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) linashiriki kwa mara ya pili katika maoenesho haya ambayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo "Madini na Fursa za Uchumi, Ajira kwa Maendeleo Endelevu" ambapo yanatarajiwa kufikia tamati Oktoba 8, mwaka huu.