NA ADELADIUS MAKWEGA
SIKU moja nilikuwa nyumbani kwangu Kijijini Chamwino Ikulu majira ya jioni sana, nilibaini kuwa sikuwa na pesa ya kufanya matumizi mbalimbali, hilo likaniladhimu nitoke nyumbani kwenda benki iliyokuwa jirani katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Chamwino.
Nilitoka kwangu kwa mguu hadi pahala pa kupanda bodaboda, nilipofika hapo kwa kuwa nilikuwa sina pesa yoyote mfukoni nilimtafuta bodaboda ninayemfahamu ili aweze kunibeba na hata nikienda benki nikikosa pesa isilete maneno na ugomvi awe mwepesi kunielewa.
Kweli nikiwa hapo bodaboda huyu ninayemfahamu hakuwepo, nilipompigia simu aliniambia anafika baada ya dakika kenda na zilipopita dakika hizo tisa alifika na kunipakia kuelekea ilipo benki hiyo.
Tukiwa njiani tulikutana na mama mmoja akitembea kwa miguu nadhani akitokea Bugiri (Njia panda ya Chamwino Ikulu) kwenda Chamwino Ikulu huku akipachika kubazi lake moja kwapani na moja likiwa limevaliwa, hili la kwapani likiwa limekatika mikanda ikining’inia mithili ya pweza aliyevuliwa pwani ya Kilindoni Mafia.
Tulimpita na tukasema labda mama huyu anaenda Chamwino Ikulu, umbali huu wa kilomita zinazokaribia 10 kwa mguu ni mwendo mrefu sana, zaidi ya saa moja, tulimuonea huruma na kupishana naye kwenda zetu benki.
Nilipofika benki, kwa bahati nzuri nilitoa pesa niliyoikuta na kumpa bodaboda huyu shilingi 10,000/- ili akate shilingi 3,000/- na nikapakia kuanza safari ya kurudi kijijini Chamwino Ikulu.
Tukiwa tunarudi tukakutana na yule mama na kubazi lake kwapani, nikamsihi bodaboda huyu anayefahamika kama Joseph, nikisema mwanakwetu tumbebe mama huyu ili tufike naye anapokwenda.
Bodaboda alisimama kando ya mama huyu, nikamsalimu, aliitikia, nikamuuliza unakwenda Chamwino Ikulu? Akajibu ndiyo. Nikamuomba apakie nyuma yangu ili kuepusha kumbahashia akiwa mbele yangu na tukaendelea na safari.
Tukiwa safarini nilimuuliza mama unaishi Chamwino Ikulu?Alinijibu kuwa hapana, yeye anatokea Mwanza lakini anakwenda Ikulu ya Chamwino kwenda kumuona Rais Samia Suluhu Hassan, kwani huku kwao amedhulumiwa ng’ombe zake.
Nikamuuliza huku Mwanza walishindwa kukusaidia? Alijibu kuwa imeshindikana na ndiyo maana anakwenda kumuona Rais Samia.
Nikasema sawa. Mimi nikafika pahala pa kushuka na mama akasema anashuka hapo hapo. Niliposhuka nikamuuliza mbona ulikuwa unatembea kwa miguu?
Akajibu pesa yote alitumia kwenye nauli kwa hiyo aliwaagiza wanawe wauze ng’ombe alafu pesa wamtumie akiwa njiani, kwa hiyo akichaji simu atawasiliana na wanawe ili aweze kupata fedha za matumizi na za nauli ya kurudi Mwanza akishamuona rais.
Kumbuka boda boda nilimpa shilingi 10,000/- pale benki , nikamwambia mpe mama huyu shilingi 3000/- atengeneze makubazi yake ni aibu kwenda Ikulu akiwa na kubazi kwapani.
Mama huyu akasema asante na huku akiomba tumuoneshe duka la dawa anunue dawa za kupunguza maumizi za shilingi 500/- akapewa noti ya 10,000/- akanunua dawa hizo duka jirani na huku akiomba achajiwe simu yake ya tochi na akarudisha chenji kwa bodaboda.
Tukiwa naye pale mama huyu nikamuuliza una hakika mheshimiwa rais yupo? Mama huyu akajibu ndiyo, akisema nilisikia katika redio yupo Dodoma na ndiyo maana amekuja kwa kushitukiza na pesa pungufu.
Nikamuelekeza ramani ya Chamwino ilivyo mimi nikapewa pesa yangu iliyobakia shilingi 4000/- nikaenda zangu kwangu na yeye akabaki anachaji simu na bodaboda akaendelea kuwasaka wateja wengine.
Baada ya siku moja mimi nikasafiri kwenda Zanzibar, huku nikiambiwa kweli simu yake mama huyu ilipopata chaji alitumiwa pesa na kukaa Kijijini Chamwino Ikulu kwa siku kadhaa bali sifahamu kama mama huyu alimuona mheshimwa huyo au la hilo mwanakwetu sikujaliwa kulifahamu.
Siku ya leo nataka kusema nini? Wakati wa Utawala wa Mwalimu Julius Nyerere kumuona kiongozi huyu kidogo ilikuwa kazi kubwa sana lakini Rais Ali Hassani Mwinyi ukiweka kando yale anayoyalalamikiwa katika utawala wake, Rais Mwinyi alijitahidi mno kujenga ujirani wa Urais wake na Watanzania.
Nakumbuka alikuwa akisikiliza malalamiko ya wananchi mmoja mmoja kila baada ya muda fulani pale Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba- Dar es Salaam na Watanzania walijaa kupeleka malalamiko yao.
Nalikumbuka hilo kwa kuwa wakati huo mimi nilikuwa mwanafunzi wa shule ya Msingi Mnazi Mmoja inayotazamana na ofisi hii na huo ulikuwa wakati wa chama kushika hatamu.
Rais John Magufuli akiwa hai alijitahidi sana kutoa nafasi ya mabango ambapo wananchi waliweza kunyanyua sauti zao, vilio vyao japokuwa si kweli kwamba yale yote yaliyokuwa mioyoni mwa Watanzania yaliweza kuandikwa katika mabango au yale mabango yote yaliruhusiwa kuonekana na kutatuliwa kero hizo.
Wengine wakidhihaki yale yaliyolalamikiwa na Watanzania kwamba mengi yalikuwa si ya kweli katika mikutano hiyo.
Labda yalikuwa ni ya mahakama na taasisi zingine. Mwanakwetu Ifahamike wazi kuwa yawe ya kweli yawe ya uwongo, yawe yamefanyiwa kazi au laa wenye nchi yao walimwambia rais wao, sawa na baba/mama (mzazi) anapoambiwa jambo lolote na mwanae.
Hiyo ni haki ya mwana kwa mzazi wake. Mzazi ndiyo anawajibu wa kupima jambo lifanyiwe kazi namna gani siyo mtu mwingine yoyote.
Hoja kubwa ni kwamba mtu anaweza akawa anamlalamkiia yule ambaye amepewa dhamana ya kusikiliza hayo malalamiko kiwilaya, kimkoa,kiwizara au kitaasisi yoyote ya umma je inakuwaje?
Kwa hiyo kwa hekima ili kusikia wenye nchi yao wanashinda gani ninashauri kinachoweza kufanyika kwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanapokwenda pahala popote wanaweza kuwatangazia umma kuwa kesho rais/ makamu / waziri mkuu atapokea malalamiko ya mwananchi mmoja, uso kwa uso, bila bughuza yoyote ile kwa saa 5 kuanzia labda saa 2-7 mchana ndani ya ofisi ya mkoa, akishazungumza na mtu mmoja mmoja ndipo ufanyike mkutano wa hadhara.
Ili zoezi hilo liwe na haki na uwazi wasimamizi wa zoezi hilo wawe wasaidizi wa Rais.Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wenyewe aliyotoka nao katika msafara wake makamo makuu na wale watendaji wa vyombo vya mkoa husika wasiwabughuzi wananchi kwenda hapo na wasiulizwe wanakwenda kuongea nae nini kiongozi wao.
Mtoto anapokwenda kuongea na baba/mama yake haulizwi anakwenda kuzungumza naye nini na mjomba au shangazi.
Kwa sasa mikutano inafanyika sana lakini ina kasoro kubwa wanaopata nafasi ni wakubwa tu na mikutano mingi mambo mengi yanatoka kutoka kwa wakubwa kwenda kwa wananchi huku wenye mkutano huo wanakuwa wasikilizaji wa hotuba tu.
Kama litafanyika hivyo jambo hilo litasaidia mno kupunguza malalamiko mengi, mabango mengi ya moyoni na safari ndefu kama za mama huyu niliyekutana naye na kubazi kwapani, akisafiri anaumwa, huku akiwa hana pesa za kutosha, akiuza ng’ombe wake nia amuone mheshimiwa.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
NB: Kwa wale wapenzi wa lugha ya Kiswahili Fasaha wafahamu kuwa neno KUBAZI/KUBADHI yote ni maneno sahihi katika lugha hii.