NA MWANDISHI WETU
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam,Mheshimiwa Prof.Kitila Mkumbo amewashauri wadau wa habari nchini kujipanga ili watakapoitwa kwenye kamati waweze kutoa hoja nzuri na zenye mashiko kuhusu mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 kwa ustawi bora wa tasnia ya habari nchini.
“Wadau wa habari wanapaswa kujipanga ili watakapokuja kwenye kamati husika waweze kutoa hoja zao kwa nini wanataka baadhi ya vifungu katika Sheria ya Huduma za Habari 2016 viboreshwe.
“Unafahamu kwenye kamati ndio wadau wanapata nafasi ya kutoa hoja zao, kwa nini wanataka baadhi ya vipengele vifanyiwe marekebisho.
Prof.Mkumbo ameyasema hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hii bungeni jijini Dodoma, baada ya kuomba kupata maoni yake kuhusu mchakato wa mabadiliko ya sheria hiyo iliyotungwa mwaka 2016.
Amesema, kwa kawaida wadau wa habari watakutana na huko ndipo wanapaswa kueleza hoja zao kwa nini wanadhani baadhi ya vifungu hivyo vinapaswa kubadilishwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Bw.Deodatus Balile akizungumzia mchakato huo amesema ingawa mpaka sasa hajajua wakati ambao mapendekezo hayo yatafikishwa bungeni, lakini bado ana matumaini kwamba safari ya mabadiliko hayo haitaishia njiani.
Balile amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan bado inaonesha kuwa na dhamira njema ya kufanya mabadiliko.
“Waziri wa Habari ndiye mwenye kujua lini watapeleka bungeni muswada, lakini sisi wadau tumepewa fursa ya kutoa maoni yetu.
“Tumeona dhamira njema ya serikali hadi hivi sasa, tukiendelea hivi nadhani huko tuendako tutashirikiana vizuri kwa maslahi mapana ya Taifa letu,”amesema Balile.