NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekutana na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mheshimiwa Yordenis Despaigne aliyefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.
Rais Dkt. Mwinyi aliishukuru Cuba kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati yake na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia sekta za elimu na afya.
Amesema Taifa hilo limekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Zanzibar kutokana na msukumo mkubwa inayotoa kupitia sekta za Afya na Elimu, ambapo pamoja na kutoa msaada wa madaktari pia hutoa fursa za masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Aidha, Dkt. Mwinyi alisema Zanziabr itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Cuba katika masuala mbali mbali ya kimataifa.
Naye Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Yordenis Despaigne alisema Cuba inajivunia uhusiano na ushirikiano wa kihistora kati yake na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, na kuahidi kuuendeleza, ili kusaidia juhudi za Serikali katika utoaji wa huduma na kuimarisha uchumi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Balozi wa Cuba nchini Tanzania,Mhe. Yordenis Despaigne alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leoSeptemba 1, 2022. (Picha na Ikulu).