NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi ameshirki katika maziko ya Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana, John Aukland Ramadhan yaliofanyika Kanisa la Anglikana Mkunazini, Mkoa Mjini Magharibi.

Katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakiwemo Mawaziri kutoka SMZ na SMT, Waziri wa Nchi (OMPR) Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma alitoa salamu za rambirambi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema wakati wa uhai wake Hayati Askofu John Ramadhan alitoa mchango mkubwa katika kuleta ustawi wa Taifa.

Waziri Hamza alisema, ana matumaini makubwa kuwa kanisa litayaendeleza yale yote aliyoyaasisi na akatumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa familia na Kanisa Anglican kwa ujumla.

Hayati Askofu Mkuu mstaafu John Ramadhan, mwenye umri wa miaka 90, alifariki dunia Septemba 12, 2022 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alikokuwa amelezwa kwa ajili ya matibabu.
