NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itaendelea kufungua milango kuwakaribisha wawekezaji kutoka nje, ili kukuza diplomasia ya uchumi na kufanikisha maendeleo ya nchi.

Amesema kuwa, milango ya Zanzibar iko wazi, salama, na ipo tayari kwa ajili ya biashara na uwekezaji, hasa kwa kuzingatia kwamba, Unguja na Pemba ni nchi yenye vivutio vingi vikiwemo vya utalii na mandhari tulivu ya kupendeza, pamoja na maeneo maalum yaliyotengwa ili kutekeleza azma hiyo.

“Kwa mfululizo tumekuwa tukipitia na kuimarisha Sera zetu za Uchumi wa Darala la Juu na wa Kima cha Chini, ili kuweza kukidhi mahitaji na matarajio ya wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza Nchini kwetu, na hata kwa wananchi wetu wenye azma ya kuwekeza,"amesema Mheshimiwa Dkt.Mwinyi.

Dkt.Mwinyi amesema kuwa, fungamano la kibiashara na kiuchumi kati ya Zanzibar na Italia ambalo ni la kihistoria, linathibitishwa na idadi kubwa ya Miradi ya Wawekezaji wa Nchi hiyo Visiwani hapa, kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambapo kwa sasa imefikia 84, ikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani 603,615,426, inayotoa fursa za ajira takriban 5,721.
Hivyo amesema kuwa katika kuhamasisha dhamira hiyo Serikali itahakikisha inayafanyia kazi mapendekezo yote muhimu kupitia kongamano hilo, ili kutoa fursa ya kukuza mashirikiano, kwa maslahi ya maendeleo ya kiuchumi baina ya Nchi Mbili hizo, na kwamba kwa mikono miwili, waje kuwekeza katika nyanja mbali mbali, zikiwemo za Uvuvi, Mazingira, Viwanda na Uchumi wa Buluu.
Kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mheshimiwa Mudrik Ramadhan Soraga, amepongeza dhamira ya Wawekezaji kutoka Utaliana kufukuzia nafasi za kuwekeza zaidi katika Visiwa vya Unguja na Pemba, hatua ambayo inaifungulia Zanzibar fursa za kujiletea maendeleo.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar (ZNCCIA), Bw. Ali Suleiman Amour, amesema kuwa Kongamano hilo la Biashara na Uwekezaji kati ya Utaliana na Zanzibar, litaimarisha daraja la mashirikiano, yakiwemo ya ushiriki wa moja kwa moja wa Sekta binfsi katika kujenga uchumi, na kwamba Serikali inao wajibu sasa wa kuweka mazingira rafiki zaidi, ili kuhamasisha mafanikio ya sekta hizo, na kwaajili ya maendeleo ya Nchi na Taifa kwa ujumla.
Balozi wa Utaliana katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Marco Lombardi, ameishukuru Serikali ya Zanzibar pamoja na Wawekezaji wa Unguja na Pemba, kwa namna walivyolipokea Kongamano hilo, na kwamba matarajio zaidi ni kuzidisha mashirikiano kati ya Nchi hizo mbili, kupitia biashara na uwekezaji, na hatimaye kufanikisha lengo la kujikwamua kiuchumi.
Tags
Fursa za Kiuchumi Tanzania
Habari
Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA)
Uchumi na Biashara
Yajayo Zanzibar Yanafurahisha
Zanzibar