NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali.
Mosi, Mheshimiwa Rais Samia amemteua, Bw. Sosthenes Laurent Kewe kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Bw. Kewe ni Mshauri Binafsi wa Uendelezaji wa Sekta Binafsi za Fedha, Dar es Salaam.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 18, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bi.Zuhura Yunus kutokea London nchini Uingereza.
Pili, Mheshimiwa Rais Samia amemteua Mhandisi Othman Sharif Khatib kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Bw Khatib anachukua nafasi ya Dkt. Jones Kilembe ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Bw. Khatib ni Mhandisi Mstaafu (TCRA).
Tatu, Mheshimiwa Rais amemteua Dkt. David Nkanda Manyanza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI). Dkt. Manyanza ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Development Solution Consultancy (T) Limited.
Nne, Mheshimiwa Rais Samia amemteua Bi. Hawa Abdulrahman Ghasia kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Shirika la Masoko Kariakoo. Bi Ghasia ni Mbunge mstaafu.
Tano, Mheshimiwa Rais Samia amemteua Bw. Sylvester Jospeh Kainda kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani. Bw. Kainda ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, uteuzi huu unaanza mara moja.