NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia upya Sheria za uwekezaji pamoja na biashara nchini ili kukabiliana na migogoro inayotokana na Sheria hizo.


Rais Samia amesema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kesi za uwekezaji, kulinda uwekezaji nchini na kupanua wigo wa kukuza uwekezaji, kukusanya mapato na hivyo kukuza uchumi kwa maslahi ya taifa.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu bila kukiuka haki za wananchi na kuwasaidia kutatua kero zao ambazo hazihitaji kufikishwa mahakamani.

Vile vile, Rais Samia amesema utoaji wa elimu utapunguza mrundikano wa mashauri ambayo hayana ulazima wa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya utatuzi na hivyo pia kuchangia kupunguza mrundikano wa mahabusu.