NA MWANDISHI WETU
KUSHUKA kwa riba kwenye hati fungani za Serikali kumeleta matokeo chanya katika soko la fedha la ndani ikiwa ni pamoja na kushuka kwa gharama za ukopaji kupitia dhamana kwa Serikali na kuanza kushuka kwa riba za mikopo itolewayo na benki za biashara, hasa kwenye sekta ya kilimo.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na mwenyeketi Mhe. Daniel Sillo (Mb) wakifuatilia semina ya BoT katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Meneja Msaidizi Idara ya Masoko ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Liku Kamba, wakati akiwasilisha mada kuhusu mwenendo wa uuzaji wa Hati fungani za serikali baada ya mabadiliko ya riba kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti jijini Dodoma leo.
“Faida nyingine ni pamoja na kuongezeka kwa mikopo itolewayo na benki za biashara kwa sekta binafsi, kukua kwa soko la hati fungani za makampuni na za halmashauri ya miji na majiji, na kuongezeka kwa biashara ya hati fungani katika soko la hisa na mitaji,”alisema.
Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila, akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati wa semina iliyofanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Alisema kuwa riba katika Dhamana za Serikali hutumika kama riba elekezi za kukopeshea kwenye sekta binafsi na vipo viashiria vinavyoonesha kuwa wastani wa riba za mikopo itolewayo na benki za biashara na taasisi za fedha umeanza kushuka kufuatia jitihada za Serikali kushusha riba kwenye hati fungani zake.
Tangu kufanyika kwa mabadiliko ya riba, “kiwango cha kukopesha kwa benki za biashara kwenye sekta binafsi kimekua kutoka asilimia 13.4 (Aprili 2022) hadi kufikia asilimia 20.1 (Julai 2022),” alisema.
Meneja Msaidizi Idara ya Masoko ya Fedha kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Bi. Liku Kamba, akielezea jambo kuhusu Mwenendo wa Soko la Hati fungani Baada ya Mabadiliko ya Riba kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwenye semina iliyofanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Bi. Liku aliongeza kuwa, kwa kuwa riba za kukopa hutegemea riba za hati fungani za serikali kama riba elekezi, mabadiliko yaliyofanyika yatasaidia kuongezeka kwa usajili wa hati fungani za makampuni (corporate bonds) na hati fungani za halmashauri za miji na Majiji (Municipal bonds).
Semina hio ilihusisha pia uwasilishwaji wa mada kuhusu Mfumo wa Taarifa za Mikopo na utendaji kazi wa taasisi za kutoa taarifa za mikopo (Credit Reference Bureaux) iliyotolewa na Meneja Idara ya Uendeshaji Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Nkanwa Magina.
Meneja Idara ya Uendeshaji Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Nkanwa Magina, akiwasilisha taarifa kuhusu Mfumo wa Taarifa za Mikopo na utendaji kazi wa taasisi za kutoa taarifa za mikopo (Credit Reference Bureaux) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwenye semina iliyofanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Bw. Magina aliwaeleza wajumbe wa Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Daniel Sillo, kuwa Mfumo wa Taarifa za Mikopo ni utaratibu wa kubadilishana taarifa za wakopaji miongoni mwa taasisi zinazotoa mikopo, zikijumuisha benki na taasisi nyingine za fedha na kukopesha kama vile watoa huduma ndogo za Fedha, kampuni za karadha (mf. nishati ya mafuta, vyombo vya usafiri, umeme, maji n.k.).
Alisema kuwa, malengo ya mfumo huo ni kupunguza ukosefu wa taarifa kati ya wakopeshaji na wakopaji ili kuwawezesha wakopeshaji kupata historia za waombaji wa mikopo kirahisi, kujenga nidhamu na uwajibikaji katika soko la mikopo kwa wakopeshaji na wakopaji na kuchangia katika udhibiti wa vihatarishi au athari zitokanazo na mikopo katika benki ili kupunguza uwezekano wa benki kufilisika.
Meneja Idara ya Masoko ya Fedha kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Bw. Lameck Kakulu, akifafanua jambo kuhusu Dhamana za Serikali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwenye semina iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.
Katika semina hiyo, Ujumbe wa BoT uliongozwa na Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila, ambaye aliishukuru Kamati kwa kuialika BoT kutoa elimu hiyo na kuahidi kwamba watakuwa tayari kufanya hivyo kila mara wakihitajika.
Meneja Idara ya Leseni, Sera na Uendeshaji kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha BoT, Bw. Frank Aminiel, akizungumza jambo kuhusu sekta ya fedha nchini wakati wa semina kwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwenye semina iliyofanyika katika ukumbi wa bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Baada ya uwasilishaji wa mada hizo, wajumbe wa kamati walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali na kutoa ushauri kuhusu mada zote mbili kwa lengo la kuboresha masuala husika.