NA GODFREY NNKO
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema, ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika ngazi mbalimbali ikiwemo nafasi za uwakilishi ni hatua moja wapo muhimu itakayochochea ufanisi katika biashara zinazoendeshwa na kundi hilo barani Afrika.
Ameyasema hayo leo Septemba 14, 2022 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi wakati akifunga Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika.
"Kauli mbiu ya mkutano huu ilikuwa ni Wanawake na Vijana: Injini ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika. Hii ni kauli mbiu nzuri kabisa na ninaomba kuwashukuru na kuwapongeza wote walioshiriki katika kuibuni na kuipendekeza,"amesema.
Pia amesema, imani yake kwamba siku tatu walizokuwepo katika katika mkutano huo watakuwa wameanza kutekeleza kauli mbiu hiyo.
"Nina imani kwamba, katika siku zote tatu mlizokuwepo hapa, mtakuwa mmeanza kuitekeleza kauli mbiu hii bila ya shaka. Hii ni kauli mbiu inayoishi na kama tukiendelea kuitekeleza kwa vitendo tutaona wanawake na vijana wengi zaidi wakishiriki na kunufaika katika biashara na hivyo kupelekea uchumi wetu kuzidi kukua na kuimarika, ikiwa ni pamoja na ajira.
"Wito wangu kwetu sote ni kwamba tuendelee kuitekeleza kauli mbiu hii kwa vitendo hata baada ya mkutano huu, kwani ni dira muhimu sana kwa wanawake na vijana wetu kote barani Afrika,"amesema Mheshimiwa Othman kwa niaba ya Rais Dkt.Mwinyi.
Pia amesema,anatarajia maazimio yote yaliyofikiwa katika mijadala yatafanyiwa kazi na Sekretarieti ya AfCFTA kwa kushirikiana na nchi wanachama.
"Maazimio haya, yatakuwa msingi na chachu ya ushiriki wa wanawake na vijana wengi zaidi katika shughuli mbalimbali za biashara barani Afrika na duniani kwa ujumla.
"Ni imani yangu pia kuwa, katika mkutano huu yamepatikana mapendekezo mahsusi ambayo yatasaidia katika uandaaji wa Itifaki ya Wanawake na Vijana ambayo inategemewa kuwainua wanawake na vijana katika biashara chini ya Eneo Huru Biashara la Afrika.
"Itifaki hii inatarajiwa kusaidia kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana katika kutumia fursa zinazotokana na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika. Kwa hivyo, natumia nafasi hii kuwaomba wanawake na vijana wa Afrika kuhakikisha kwamba mnatumia vyema fursa zinazopatikana katika Bara la Afrika na kwa manufaa ya nchi zetu za Afrika kwa kuzingatia utajiri tulio nao,"amesema.
Makamu wa Rais wa Kwanza alitumia nafasi hiyo kuzipongeza na kuzishukuru nchi zote za Afrika kupitia Sekreterieti ya Eneo Huru la Biashara la Afrika, kwa heshima kubwa waliyoipatia Tanzania.
"Ni kwa kumuamini Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumteua kuwa Kinara na Mhamasishaji wa Wanawake na Vijana katika Biashara Afrika. Ninawahakikishia kuwa, hamkukosea kwani mnaamini kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania atatekeleza kwa umahiri mkubwa jukumu hilo la kuwahamasisha wanawake na vijana katika Biashara Barani-Afrika kwa vile ana ushawishi mkubwa na uzoefu katika masuala kama haya ya maendeleo,"amesema.
UNDP
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi.Christine Musisi amesema, huu umekuwa mkutano wa aina yake ambao umeleta hamasa na kuibua changamoto mbalimbali zinazohusiana na biashara zinazowahusu wanawake na vijana.
Musisi amesema kuwa,kupitia maazimio ya mkutano huo utatoa dira kwa viongozi wa Afrika kwenda kuandaa sera na mipango ambayo itakuwa rafiki kwa ajili ya kuinua na kuboresha biashara hizo kwa manufaa ya jamii na Taifa.
"Wanawake ni nguzo kuu. Nguzo hii inafanya kazi, hivyo tunaamini kupitia sera nzuri na endelevu zitasaidia kuwajengea mazingira bora ambayo utekelezaji wake utatoa majawabu muhimu kwa mustakabali wa uchumi endelevu katika jamii na bara la Afrika kwa ujumla.
"UNDP na UNWomen tupo tayari kusaidia na kufanikisha mipango yote ambayo imedhamiria kuinua biashara zinazoongozwa na wanawake, hivyo kuwapa dira ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara,"amesema.
Pia amesema, wapo tayari kufanya kazi na wanawake ikiwemo sekretarieti hiyo ili yale yaliyojadiliwa katika mkutano huo yaweze kuingia katika utekelezaji kwa haraka yaweze kuleta ufanisi kwa manufaa ya wanawake na vijana barani Afrika.
Waziri
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar, Mheshimiwa Riziki Pembe amesema kuwa,wizara zote mbili zinaunga mkono juhudi zilizochukuliwa na Bara la Afrika katika kuwakomboa wanawake na vijana kiuchumi.
Amesema, hiyo ni sehemu ya kimkakati katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza ili Taifa likuwe kiuchumi, kundi hilo lazima pawepo ushirikishwaji katika uundaji wa sera za uchumi na kutengewa bajeti katika suala zima la jinsia.
Sambamba na kusaidia ushiriki wa biashara ndogo za kati na kubwa kwa wanawake na vijana ili kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana miongoni mwa kundi hilo na Taifa kwa ujumla.
"Kwa hiyo, kuwa, katika biashara katika makundi hayo yote kwa lengo la kuona kwamba wanawake na vijana wanashiriki katika maendeleo katika bara letu la Afrika na kuyafikia masoko, kitaifa, kikanda na Kimataifa ikiwa ni pamoja na kushiriki katika majadiliano ya kibiashara.Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi yupo mstari wa mbele katika kuhakikisha hifadhi na maendeleo ya kundi la wanawake na vijana yanapatikana kwa haraka,"amesema.
Waziri Said
Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said amesema,mkutano huo umefanyika katika kipindi mwafaka kwani, umuhimu wake si tu kwamba umeangalia changamoto zinazowakabili wanawake na vijana lakini pia umewaleta vijana wenyewe katika mjadala.
"Hilo ni jambo muhimu sana, uzoefu unaonesha katika bara la Afrika,watunga sera wanajifungia wenyewe, wanajadili kwa niaba ya watu wake na kwa niaba ya vijana, lakini kitu kizuri katika mkutano huu umewaleta pamoja makundi ya vijana na wamekuwa wakijadili changamoto,ni matumaini yangu baada ya mkutano huu Sekretarieti ya AfCFTA itayachukua maazimio, kwa kwa kushirikiana wawakilishi wa Serikali katika mkutano huu kwenda kuyafanyia kazi,"amesema.
AfCFTA
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), Wamikele Mene amesema kuwa, wameyapokea maazimio ya mkutano huo ambayo yametokana na maoni na hoja mbalimbali walizoibuwa washiriki wa mkutano huo ili yaweze kufanyiwa kazi.
"Tumeyapokea maazimio na maoni mbalimbali ya wanawake na vijana kuanzia siku ya kwanza ya mkutano hadi leo hii tunapohitimisha, hivyo Sekretarieti inaahidi kwenda kuyafanyia kazi ikiwemo vikwazo na changamoto ambazo zinawakabili katika biashara zao. Lengo ni kuhakikisha wanawake na vijana wanafanya biashara kwa manufaa ili ziweze kuwakomboa wao na kukuza uchumi wa mataifa yao,"amesema Mene.
Mkutano huo wa siku tatu ambao ulianza Septemba 12, 2022 ukiwakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania ukiongozwa na kauli mbiu isemayo Wanawake na Vijana: Injini ya ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (Women and Youth: The Engine of AfCFTA Trade in Africa) ambapo umehitimishwa leo Septemba 14, 2022.