Serikali yataja mikoa iliyopo hatarini kupata ugonjwa wa Ebola

NA DIRAMAKINI 

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu leo Septemba 28, 2022 ametaja mikoa iliyopo katika hatari ya kupata mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Tahadhari hiyo imekuja ikiwa ni siku nane tangu kutokea mlipuko wa ugonjwa huo Septemba 20, 2022 katika Wilaya ya Mubende nchini Uganda ambapo mpaka sasa tayari vifo 23 vimetokea.
Waziri Ummy amesema mikoa ambayo iko hatarini kupata maambukizi ni Kagera, Mwanza, Kigoma, Geita na Mara.

Ameongeza kuwa, mikoa ya Dar Es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya na Dodoma ipo katika hatari kwa sababu ya uwepo wa viwanja vya ndege na vituo vikubwa vya mabasi.

Waziri Ummy amewaagiza wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha wanajiandaa ipasavyo ikiwa itatokea mgonjwa mwenye dalili za Ebola wapi atatengwa ili kutibiwa, timu ya wataalamu, ambulance na eneo la maziko iwapo kifo kitatokea.

“Kwa mamlaka niliyopewa nawaagiza wakuu wa mikoa kote nchini kila mkoa kujiandaa na ni lazima waainishe ni gari lipi la wagonjwa ‘ambulance’ itatumika, timu ya wataalamu wa afua, mtu wa maabara ni yupi na mgonjwa akipatikana anapelekwa wapi, kuhakikisha kuna vifaa na atapelekwa wapi.

"Hadi sasa hakuna mgonjwa wa Ebola nchini, hivyo yatupasa kila mmoja wetu kuchukua hatua na kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini.

"Dalili kuu za ugonjwa wa Ebola ni homa kali, mwili kuchoka, kuumwa viungo vya mwili, vidonda kooni, kuhara na kutokwa damu katika matundu ya mwili," ameeleza Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema, ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yanayosambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kwa kula au kugusa mnyama mwenye maambukizi kama nyani, kima, popo na swala.

"Ugonjwa wa Ebola unaenea kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine kwa kugusa majimaji ya mwili wa mgonjwa kwa mfano mate, machozi, damu, matapishi, mkojo na kinyesi. Endapo mtu ataona dalili hizi awahi kituo cha kutolea huduma za afya," amefafanua Waziri Ummy.

Aidha, ametoa maelekezo kwa jamii kusitisha safari zote hasa kuepuka kutembelea maeneo hatarishi yenye ugonjwa, kula nyama ambayo haijapikwa vizuri, kuepuka kugusa mate, machozi na kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news