NA TITO MSELEM
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO), limepunguza utegemezi kutoka Serikalini ili lijiendeshe kwa fedha zake ambapo utegemezi umeshuka kutoka asilimia 89 Mwaka 2018/19 hadi asilimia 9.2 Mwaka 2022/23.Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Ollal wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye kikao kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.
Ollal amesema , STAMICO imeweza kuanzisha miradi yake kutokana na fursa mbalimbali zinazojitokeza ili kuongeza vyanzo vya mapato ya ndani na kupunguza utegemezi Serikalini ili Shirika lijiendeshe kubiashara.
Ollal amesema mapato ya Shirika yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 5.86 kwa Mwaka wa Fedha 2019/20, shilingi bilioni kwa 19.6 Mwaka wa Fedha 2020/21 na shilingi bilioni 48.5 kwa Mwaka wa Fedha 2012/22.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Vanance Mwasse amesema baada ya changamoto ya kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta, Shirika limeangalia namna bora ya kulipa deni lake ambapo mpaka sasa Shirika limelipa zaidi ya shilingi bilioni 1.7 na linategemea kuanza kulipa shilingi milioni 600 kila mwezi mpaka deni litakapomalizika.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nyasa Stella Manyanya amesema, Serikali iangalie namna ya kulisaidia Shirika kulipa mkopo wa shilingi bilioni 18.75 ili wadai mbalimbali wapate haki zao na kufanya biashara zao baada ya kulidai shirika hilo kwa muda mrefu.
Pia, Mbunge wa Jimbo la Ulanga Salim Hashim ameitaka Serikali kuangalia namna ya kuziongezea Halmashauri mapato yatokanayo na Sekta ya Madini ambapo amesema tozo zitokanazo na mrabaha ambayo ni asilimia 7 ipunguzwe kwa asilimia 2 ili asilimia 5 iende Serikali Kuu a asilimia 2 ibaki kwenye Halmashauri husika.
Aidha, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameishukuru Kamati hiyo kwa maagizo iliyoyatoa na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo hayo yenye lengo la kuiboresha Sekta ya Madini.
“Wizara ya Madini tutaendelea kufanyia kazi maelekezo na ushauri wa Kamati ili kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na hatimaye kufikia mchango wa asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.