Tanzania,Iran kujenga Chuo Kikuu cha Kiswahili nchini

NA JOHN MAPEPELE

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekubaliana kujenga Chuo Kikuu cha Kiswahili nchini ikiwa ni mkakati wa kuimarisha mahusiano mazuri katika eneo la utamaduni baina ya nchi hizo.
Makubalino hayo yamefikiwa Septemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam katika kikao baina ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa na ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al- Mustafa Iran ulioongozwa na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mhe. Hossein Alvandi Bahineh.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu hicho ambacho kitasaidia kubidhaisha lugha adhimu ya Kiswahili duniani kwa kupata wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani.

Amesema kutokana na umuhimu wa lugha hiyo Shirika la Utamaduni duniani ( UNESCO) limeipitisha lugha hiyo kuwa ni miongoni mwa lugha itakayokuwa ikitimika katika mikutano ya kimataifa.

Aidha, amesema kwa sasa lugha hiyo inatumiwa na zaidi ya watu milioni 250 duniani kote na kufundishwa kwenye vyuo vikuu maarufu duniani.
Amesema kwa sasa wanasubiri kutiliana saini makubalino hayo baada ya kila pande kupitia mikataba hiyo katika kipindi kifupi kijacho.

Ameongeza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na utajiri wa tamaduni nzuri ambazo zimeota mizizi kutokana na usimamizi thabiti kuanzia kuasisiwa taifa hili na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Marais wote hatimaye Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya mageuzi makubwa kwenye lugha hiyo hadi kutambulika kuwa lugha rasmi kimataifa na kupewa siku maalum ya kuiadhimisha ambayo ni Julai 7, ya kila mwaka.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na UNESCO katika kuhakikisha Kiswahili kinabidhaishwa na kutumia duniani kote.
Rais wa Chuo hicho, amesema kwa sasa Chuo tayari kinafundisha lugha za kimataifa 17 za nchi mbalimbali duniani ambapo pia baada ya kukamilika ujenzi wake lugha nyingine zitafundishwa.

Aidha, ametoa wito kwa wataalam wa Tanzania kwenda Iran kwa ajili ya kujifunza na kubadilisha uzoefu katika eneo la utamaduni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news