TEA yawashika mkono mabinti shuleni kupitia Kampeni ya Namthamini

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imeunga mkono Kampeni ya Namthamini inayoratibiwa na Kituo cha Runinga cha EATV jijini Dar es Salaam kwa kutoa taulo za kike pakiti 1,500 zenye thamani ya shilingi milioni 1.5.
Mchango huo umewasilishwa kwa uongozi wa EATV jijini Dar es Salaam leo Septemba 29, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bi.Bahati I. Geuzye kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji shuleni.

"Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na nafasi ya kukutana hapa kwa ajili ya kampeni maalum ijulikanayo kama ‘‘NAMTHAMINI’’ inayolenga kuchangisha taulo za kike kwa wanafunzi wenye uhitaji mashuleni.
"Pia natoa shukrani za kipekee kwa Uongozi wa EATV kutambua na kuona changamoto zinazowakabili watoto wa kike hasa wanaotoka katika mazingira magumu na kuwafanya washindwe kuhudhuria na kufurahia masomo wanapokuwa shuleni,

"Leo tuko hapa kukabidhi taulo hizi za kike jumla ya boksi 62 zenye thamani shilingi milioni 1.5 inayojumuisha mchango wa taasisi na michango ya watumishi wa TEA. Tunawaahidi kuendelea kuunga mkono kampeni hii tukitambua umuhimu wake na tunahamasisha taasisi zingine na watu binafsi kujitokeza kuchangia taulo hizi za kike kwa wanafunzi wenye uhitaji mashuleni.

"Ni matumani yetu kuwa ushirikiano wetu wa karibu na EATV utaongeza na kuinua upatikanaji wa elimu bora kwa usawa nchini kote,"amebainisha Bi.Geuzye.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, Mamlaka ya Elimu Tanzania inatambua mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa kike yana changamoto nyingi ambazo zinawafanya wakose fursa ya elimu bora na kwa usawa.

"Katika barua yenu mliyotuandikia mlieleza kuwa tafiti nyingi zinaonyesha wasichana wengi hapa nchini hukosa masomo kwa wastani wa siku 60 kwa mwaka wanapokuwa katika hedhi kutokana na ukosefu wa taulo za kike.

"Kwa kuliona hilo, TEA inaungana na ninyi katika kampeni ya NAMTHANIMI, kwa kuchangia taulo za kike ili kuwasaidia watoto hao waweze kuhudhuria masomo na kupata elimu bila vikwazo na hatimae wazifikie ndoto zao kwani ukimuelimisha mwanamke, umeelimisha jamii kwa ujumla,"amesema.
Amefafanua kuwa, Mamlaka ya Elimu Tanzania ni taasisi ya umma inayofanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Bi.Geuzye amesema, TEA ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001 chini ya kifungu 5 (1) pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2013 kwa lengo la kuratibu uendeshaji wa Mfuko wa Elimu, ambao pia ulianzishwa kwa Sheria hiyo Na.8 ya mwaka 2001, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa nchini.
"Kama nilivyosema hapo awali, TEA inatekeleza majukumu mbalimbali lakini jukumu mojawapo ni kusaidia jitihada za Serikali kuongeza upatikanaji wa Elimu bora na kwa usawa kwa kuhakikisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia yanaboreshwa na kuwa rafiki kwa watoto wote wa kike na kiume.

"Naomba niwapongeze tena EATV kwa kuunga mkono jitihada hizi za Serikali za kuboresha miundombinu ya elimu na kuanzisha kampeni hii ya NAMTHAMINI ya kuchangisha taulo za kike kwa wanafunzi wenye uhitaji mashuleni ili kuwafanya wanafunzi hao wasikose masomo pindi wanapokuwa katika hedhi,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu huyo.
"Aidha, shukrani za pekee ziende kwenu EATV kwa kuwa washirika wetu wakubwa katika uhabarishaji ambapo kupitia ushirika huo tumeweza kushiriki kampeni ya NAMTHAMINI inayolenga kusaidia watoto wa kike kuhudhuria masomo hasa wanapokuwa kwenye hedhi,"amesema Bi.Geuzye.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news