'Tunampongeza sana kwa jitihada zake hizo na leo tunakukaribisha wewe mwenyewe kuona maendeleo ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi'

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba amewapongeza wanaushirika wa Kikundi cha Kumekucha kilichopo Shehia ya Mzuri Makunduchi kwa kuzitumia vyema fedha za mkopo wa Uviko-19 na kuweza kuendeleza kilimo cha mbogamboga ambacho kinawapatia tija na kujikwamua kimaisha.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini ametoa pongezi hizo huko katika shamba la Ushirika wa Kumekucha lililopo Shehia ya Mzuri Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kuzindua uvunaji wa tungule (nyanya) huko katika shamba la ushirika huo.

DC Mkasaba alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuwakumbuka wajasiriamali na kuwawekea fedha nyingi ili waweze kukopa na kuendesha shughuli zao za kimaendeleo.
Amesema kuwa, ushirika huo umeonesha mfano mkubwa wa kuthamini fedha za mkopo ambazo wameweza kuzifanyia mradi mkubwa wa kilimo cha mboga mboga.

Amewahakikishia Wanaushirika hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi itaendelea kuwaunga mkono wajasiriamali wote ili kuhakikisha wanafikia lengo walilolikusudia katika kupambana na umaskini na kujikwamua kiuchumi.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini aliwasisitiza Wanaushirika hao waendelee kushirikiana ili waweze kupata maendeleo makubwa zaidi katika ushirika wao.

Sambamba na hayo, aliwaeleza kwamba iwapo wataendelea na juhudi zao hizo walizozichukua katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kujikusanya pamoja na kuunda ushirika huo na kuweza kuomba mkopo na kuutumia vizuri, kuna uwezekanao mkubwa wa kupewa kipaumbele pale watakapomaliza mkopo na kuamua kukopa kwa mara nyingine tena.

Akisoma risala ya Ushirika huo kwa Mkuu wa Wilaya, Bi.Rehema Issa Ameir ambaye ni miongoni mwa Wanakikundi cha Kumekucha alisema kuwa mnamo Juni 6,2022 waliweza kupata mkopo ambao ulizinduliwa na Rais Dkt.Mwinyi.

Hivyo, Wanaushirika hao walimpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa juhudi zake hizo ambazo zimewapelekea hivi sasa kuanza kuonja matunda yake.

“Tunampongeza sana kwa jitihada zake hizo na leo tunakukaribisha wewe mwenyewe kuona maendeleo ya Dkt.Hussein Ali Mwinyi,”alisema Bi.Rehema.

Akieleza historia fupi ya Ushirika huo, Bi Rehema alisema kuwa Ushirika huo ulianzishwa Machi 3, 2012 ukiwa na wanachama 20 ukianzia na shughuli za kilimo cha migomba kwa muda na baadae wakaona haja ya kuingia katika kilimo cha mboga mboga ambacho hadi leo wanaendelea nacho.
Pamoja na hayo, Wanaushirika hao walieleza changamoto waliyonayo ambayo ni kukosa umeme wa uhakika na usio salama kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kilimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news