TUSIMAMIE HAKI ILI KULETA MAENDELEO KATIKA NCHI-MHE.OTHMAN

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kukosekana kwa mfumo wa haki unaopelekea kuwapata viongozi imara na wanaostahiki kuiongoza nchi, ni moja ya mambo yanayokwamisha juhudi za wananchi kuyafikia maendeleo ya kweli.
Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti, katika mwendelezo wa ziara yake ya ujenzi na uimarishaji wa chama, alipotembelea Majimbo ya Chaani na Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema kuwa, mfumo huo ni ule ambao unatokana na uwepo wa taasisi imara zinazoweza kuasisi utaratibu wa kuwapata viongozi wanaoridhiwa na umma na kupata ridhaa ya kuiongoza nchi, kwa kufuata misingi ya haki, heshima na uadilifu.

Mheshimiwa Othman amezitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na zile zinazoaminika katika kulinda kwa uadilifu raslimali, mali za umma na haki za wananchi wote bila ubaguzi, zikiwemo mamlaka za kusimamia sheria na tume za uchaguzi.
Akiongea na viongozi, wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo katika Majimbo hayo, Mheshimiwa Othman ameeleza dhamira ya chama hicho kuendeleza harakati ambazo msingi wake ni upatikanaji wa taasisi hizo ambazo hatimaye zitasimamia juhudi na matumaini ya umma, katika kufikia Zanzibar wanayoihitaji na maendeleo wayatakayo.

“Hatutoweza kuitekeleza dhamira hiyo bila ya kushikamana na kuunga mkono kwa pamoja juhudi za kujenga na kuimarisha chama imara ili hatimaye tuweze kufikia Zanzibar tuitakayo,"amesema Mheshimiwa Othman.
Akiongelea juu ya changamoto mbali mbali zilizowasilishwa na wananchi, zikiwemo uporwaji wa ardhi na mashamba ya watu wa Kijiji cha Kandwi, Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Mheshimiwa Othman ameahidi kwamba dhuluma ya aina yoyote haiwezi kupuuzwa, na kwamba lazima kuwepo na utaratibu ambao yeye binafsi atausimamia kuhakikisha haki inatendeka.

Viongozi mbalimbali na watendaji wa chama hicho wamejumuika katika ziara hiyo, wakiwemo Wenyeviti na Makatibu wa Mikoa, Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya ACT-Wazalendo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news