Wadau wa uhifadhi mfumo wa ikolojia hewa ya ukaa ya bluu na uendelezaji wa uchumi wa bluu wakutana

NA HAPPINESS SHAYO-WMU

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amefungua warsha ya siku mbili ya wadau wa uhifadhi mfumo wa ikolojia wa hewa ya ukaa ya bluu na uendelezaji wa uchumi wa bluu Tanzania, lengo ikiwa ni kujadili namna bora ya kuondokana na changamoto zinazoikabili sekta ya misitu nchini.
Warsha hiyo imefunguliwa Septemba 27,2022 katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Mhe. Masanja amesema misitu ya mikoko na majani ya baharini inatarajiwa kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa bluu kwa kuhifadhi hewa ya ukaa mara tano zaidi ya misitu ya kawaida.
Ameelekeza washiriki wa warsha hiyo kuibua masuala muhimu yatakayoisaidia Serikali kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya biashara ya hewa ya ukaa.

Ametaja faida nyingine za misitu ya mikoko kuwa ni kusaidia kukabiliana na athari za kimazingira kama mabadiliko ya tabia ya nchi, mmomonyoko wa udongo na vimbunga baharini, kusaidia uwepo wa mazalia ya samaki, chanzo cha kuni, mbao na milunda ya kujengea.
Aidha, amesema uwepo wa shughuli za kibinadamu katika misitu ya mikoko, hupelekea kupotea kwa mikoko na kuathiri ukuaji wa uchumi wa bluu.

Mhe. Masanja amefafanua kuwa ili kukabiliana na changamoto za upotevu wa misitu ya mikoko Serikali itatoa elimu kwa wananchi namna bora ya kutunza mikoko hiyo na kushiriki moja kwa moja katika uhifadhi wa mikoko kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Huduma za Misitu za Misitu Tanzania, Prof Dos Santos Silayo amesema wananchi wanatakiwa wawe na mifumo endelevu ya kupata kipato itakayowawezesha kukidhi mahitaji yao bila kukata mikoko.

“Mifumo hii itawawezesha wananchi kuvuna hewa ya ukaa na kujipatia fedha bila kuathiri mikoko kwa mfano kufanya shughuli za ufugaji nyuki na utalii,”amefafanua Prof. Silayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uvuvi, Wizara ya Uchumi wa Bluu Zanzibar, Dkt. Salumu Hemedi amesema kuna uhusiano mkubwa wa uchumi wa bluu na biashara ya hewa ya ukaa.

Amesema biashara ya hewa ya ukaa inafanyika sana katika mataifa mengi duniani ambayo yana viwanda yanatumia hewa ya ukaa katika nchi ambazo zina misitu ambazo zinalipwa ili kutunza misitu.
Warsha hiyo imehudhuriwa wa Maafisa kutoka Serikali ya Tanzania na Kenya, Wawakilishi wa Sekta Binafsi, Wadau wa Uhifadhiwa Mifumo Ikolojia ya Bluu pamoja na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news