NA DIRAMAKINI
WANANCHI mbalimbali mkoani Mara wamejitokeza kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kudhibiti vikali vitendo vya ujambazi ambavyo vilianza kushamiri mkoani humo hivi karibuni.
Wananchi hao wameelezea namna vitendo vya uhalifu wa silaha za moto ambavyo hutekelezwa na baadhi ya ndugu na wanafamilia wenzao katika kaya mbalimbali vinavyoathiri biashara na kufilisi mali za wakaazi wa mkoani humo.
"Wananchi wanaishi kwa hofu, wafanyabiashara wanafilisiwa mali zao, wanavunja majumba ya watu usiku na kukosesha watu amani wakiwa na silaha, na wengine tunaishi nao na tunawafahamu hivyo tunashukuru Jeshi la Polisi hata kuwaua kwetu ni furaha tosha,"amesema Yusuph Wambura ambaye ni kiongozi wa vikundi vya ulinzi wa jadi mkoani humo almaarufu kama 'Litongo'.
Vilevile, mwananchi aliyefahamika kwa majina ya Mugale Chacha, ambaye ni ndugu na jambazi aliyepoteza maisha katika tukio la mapambano ya kurushiana risasi na askari polisi hivi karibuni naye amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuzidisha ulinzi na kuchukua taarifa za viongozi wa vijiji kwani ndugu yao huyo ameshajadiliwa sana katika vikao vya kiukoo ili kumdhibiti na tabia ya ujambazi wa kutumia silaha bila kukoma.
"Ndugu yangu Mugale ambaye amepoteza maisha kwa vitendo vya ujambazi tulishamuasa sana aachane na vitendo hivyo, lakini mpaka mauti yanamkuta ni kweli jamii ilishamchoka, walishafungwa gereza la Butimba na taarifa zao zipo, vifungo kadhaa ila bado wanatoka wanarudi uraiani, hivyo sisi Mugale tulishamchoka kwa historia na vitendo vyake vya uhalifu na alikuwa anamiliki silaha za moto za kufanyia uhalifu,"amesema.
Wakati huo huo, wananchi hao wametumia nafasi ya kuongea na mwandishi wetu kuwaomba wanasiasa, kutoingiza siasa katika maslahi mapana ya wananchi ya mkoa wa Mara ama kulichonganisha Jeshi la Polisi na raia kisiasa kwa kutumia tukio la majambazi hao ambao wamesumbua sana amani na kuiba mali za wana-Mara.
"Wanasiasa waache kulichonganisha Jeshi letu la Polisi na wananchi, sisi tumefurahi majambazi hawa kudhibitiwa, na pengine Polisi wangeuawa iwapo wasingekua makini na majambazi hawa wenye silaha, hivyo tumefurahi na kiukweli tulidhani polisi labda wameshindwa kuwadhibiti majambazi mkoani humu, ila sasa tumeona kazi ya Jeshi la Polisi ikiwa imara,"amesema.
Kama hiyo haitoshi, wananchi hao wamelitaka Jeshi la Polisi kuendelea na msako wa majambazi hao, huku wakimtaja mtu mmoja aitwaye 'Barassa Barassa' kuwa ni jambazi sugu ambaye bado yupo uraiani na anapaswa adhibitiwe na Jeshi la Polisi kwa usumbufu wa wizi wa mali za raia kwa kutumia silaha mkoani humo.
"Tunaliomba Jeshi la Polisi liendelee kumtafuta Barassa Barassa, ambaye amebaki uraiani, majambazi hawa wana mnyororo mrefu sana wa matukio na washirika wao wa masuala ya ujambazi mkoani humu, huyu Barassa ndie jambazi sugu mwingine ambaye tunatamani vyombo vya dola vimtie nguvuni haraka iwezekanavyo, na sisi tuko tayari kuja mbele kuwataja wote wanaohusika na ujambazi akiwemo Barassa Barassa,"amesema.
Tags
Habari
Jeshi la Polisi Tanzania
Kataa Uhalifu Uishi Salama
Mkoa wa Mara
Tanzania Bila Uhalifu Inawezekana
Uhalifu Haukubaliki Tanzania