NA DIRAMAKINI
SERIKALI imetangaza kuanza kuchukua hatua kali kwa watu watakaobainika kusambaza maudhui yanayohamasisha mapenzi ya jinsi moja.
Pia, amewatahadharisha viongozi wa makundi ya ya WhatsApp ma ‘admin’ ambao hawatafuata au kuchukua hatua kwa wanaosambaza maudhui ya mapenzi ya jinsi moja yakiambatanishwa na video au picha kuwa watachukuliwa hatua kali pamoja na vyombo vya habari.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Septemba 11, 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye jijini Dar es Salaam.
Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kukithiri kwa vipande vya video zinazosambaa mitandaoni zikionyesha vitendo vya aina hiyo.
“Tumefuatilia kwenye vyombo vyetu ambavyo tumevipa leseni hakuna ambacho kinahusika katika hili, watu wanapakua kupitia pay tv matokeo yake zinasambaa kupitia mitandao ya kijamii hasa makundi ya WhatsApp,”amesema Nape na kuongeza.
“Sasa nitoe tahadhari tutakapoanza kuwazoa, hatutegemei taharuki maana hadi mimi kujitokeza kuzungumzia hili suala ni wazi kwamba tumeamua kulifanyia kazi. Kuweni makini huko kwenye mitandao na makundi ya WhatsApp hasa ma admin hatuna utani katika hili,” amesema. (Mwananchi)
Tags
Habari
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA
Maudhui Mabaya Mitandaoni
Sekta ya Habari na Mawasiliano