NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza wanunuzi wote ambao wamechukua tumbaku za wakulima na hawajawalipa fedha zao wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani kwani Serikali inataka kuona wakulima wakinufaika na zao hilo.
“Tumbaku katika mkoa wa Tabora ni uchumi, hivyo viongozi kuanzia ngazi ya wizara, mkoa, wilaya, kata na hata vijiji simamieni ushirika kwenye maeneo yenu, ushirika ni uchumi. Sote tuwajibike kwa pamoja, tuhakikishe ushirika unapata mafanikio.”
Ametoa agizo hilo leo mchana Ijumaa, Septemba 9, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika, AMCOS na wakulima wa tumbaku kutoka wilaya za Urambo na Kaliua, mkoani Tabora.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayebainika kuhujumu ushirika nchini kwa sababu imedhamiria kuuboresha.
Amewaagiza viongozi wa vyama vikuu vya ushirika waende kwa wakulima na kushirikiana nao kutatua matatizo yao. “Kutaneni na viongozi wa mkoa na wilaya na muwaeleze changamoto zenu, viongozi wa Serikali nanyi wapokeeni na muwasikilize.”
Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya kijiji wasimamie mwenendo wa ushirika katika maeneo yao na wahakikishe kwamba hakuna migogoro, wizi wala dhuluma kwa wakulima. “Hatua zichukuliwe kwa watakaowadhulumu wakulima.”
Amesema Mheshimiwa Rais Samia amedhamiria kuendelea kusimamia ushirika wa mazao mbalimbali likiwemo la tumbaku, hivyo amewasisitiza viongozi hao waongeze usimamizi katika ili kuimarisha maisha ya wakulima wa zao hilo.
Amesema kitendo cha viongozi wa AMCOS kwenda kwa Waziri Mkuu na kuwasilisha kero zao wakati katika maeneo yao kuna viongozi kinaonesha kwamba kuna shida, amewasisitiza viongozi wa halmashauri watekeleze majukumu yao ipasavyo.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha maafisa ushirika nchini wakamilishe agizo lake alilolitoa mwaka jana la kuandaa kanzidata ya wakulima ili kuiwezesha Serikali kuwatambua wakulima na kurahisisha utoaji huduma.
Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia anaifahamu vizuri sekta ya kilimo, ndiyo maana amefanya maboresho makubwa kwenye sekta hiyo. “Viongozi wa vyama vya ushirika hakikisheni mnakutana na wakulima mara kwa mara ili kutatua kero zao.”
Kwa upande wao, baadhi ya wakulima wa zao la tumbaku waliozungumza kwenye mkutano huo wamempongeza Rais Samia kwa kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea ambayo imewasaidia kuongeza tija katika kilimo.
Pia wameomba uwekwe utaratibu wa kuwahishwa kwa pembejeo za kilimo ili waweze kufikia malengo yao ya uzalishaji na kuwataka maafisa ugani wafike mapema kwa wakulima badala ya kusubiri wakati wa mavuno ndipo watoe kasoro.