Waziri Dkt.Mabula ataja mikoa nane iliyochelewesha taarifa za uhakiki wa mashamba

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula ameitaja mikoa nane ambayo licha ya kuagiza ufanyike uhakiki wa mashamba na apate taarifa ifikapo Julai, 2022 ambapo baadaye Katibu Mkuu, Dkt.Allan Kijazi aliongeza muda hadi Agosti 15, 2022 haijawasilisha taarifa hizo.

"Mara kadhaa kupitia vikao mbalimbali au kwa njia zingine rasmi binafsi nimeelekeza masuala mablimbali ambayo ningependa kupata taarifa zake haraka na kuzifanyia kazi. Kwenye eneo hili sijaona uharaka na uthabiti katika utekelezaji.

"Mathalani, niliagiza ufanyike uhakiki wa mashamba nipate taarifa ifikapo Julai, 2022 na Katibu Mkuu ninazo taarifa uliongeza muda hadi tarehe 15 Agosti, 2022 taarifa ziwe zimewasilishwa. Mpaka hapa tunapokongea, ni Mikoa 17 pekee ndio imewasilisha. Mikoa ambayo haijawasilisha ni Arusha, Dodoma, Geita, Kagera, Njombe, Shinyanga, Simiyu na Songwe;
Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula ameyabainisha hayo leo Septemba 6,2022 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi cha makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa 26 nchini.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, miongoni mwa makamishna hao kuna hali ya kutotambua majukumu waliyopewa.

"Makamishna wasaidizi mmeteuliwa kwa utaratibu na kwa hati rasmi zinazowaelekeza kusimamia shughuli zote za sekta kwenye ngazi ya mikoa na halmashauri kwa niaba ya wizara.

"Pamoja na kutimiza majukumu yenu, wapo baadhi yenu ambao mna mapungufu ya kuelewa nini mnapaswa kufanya, mnakosa weledi na ubunifu. Mnafanya kazi kwa mazoea, mnaogopana, mnalindana na hivyo kuathiri utendaji wetu wa kazi.

Kutokana na hali hiyo,Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amemwelezekza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi aanze kuchukua hatua mara moja kwa wale walioshindwa kukidhi matarajio pamoja na wasaidizi wao.

"Pamoja na hatua za kinidhamu ambazo zimechukuliwa kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwaachisha kazi kwa mikoa ya Mbeya watatu na Dodoma wanne,ninaagiza hatua zichukuliwe kwa mikoa mingine. Kwa mashauri ya kinidhamu ambayo yanaendelea, naelekeza yakamilishwe haraka.

"Mikoa ambayo tunakamilisha taratibu za kinidhamu kwa watumishi siku za hivi karibuni ni Mbeya, Dar es Saaam, Mwanza na Arusha na Lindi. Aidha, tumebaini kuwa wapo watumishi ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya udanganyifu kwenye zoezi la uthamini wa mali,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Pia amesema, hao wamepata majina yao na watachukua hatua haraka. "Siridhishwi kabisa na utendaji wa Mkurugenzi wa TEHAMA. Naelewa Katibu Mkuu analifanyia kazi, naelekeza lifanyiwe kazi kwa haraka na kwa muda mfupi.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, "Nimekuwa nikipokea taarifa kutoka kwenye ngazi mbalimbali za uongozi kwenye mikoa na wilaya kuhusu namna tunavyoshirikiana nao kutekeleza majukumu yetu na kutatua kero za wananchi.

"Mrejesho ni mzuri, lakini baadhi yenu ninazo taarifa za kutoshirikiana kikamilifu na viongozi wa mikoa. Nataka mkabadilike na kubadili mtazamo ya namna ya kufanya kazi. Tutambue kuwa sote tunafanya kazi kwa niaba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na majukumu yote mnayotekeleza mnapaswa kushirikiana na mamlaka za mikoa, wilaya, halmashauri pamoja na taasisi zingine ndani ya maneo mnayoyasimamia,"ameagiza Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Akizungumzia kwa upande wa weledi na ubunifu, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema kuwa, "Kama nilivyoeleza hapo awali, nyie ndio jicho la wizara kwenye kusimamia misingi ya uwajibikaji, weledi na uadilifu kwenye ngazi ya mkoa na halmashauri.

"Nimeanza kupokea taarifa za baadhi yenu kushiriki au kwa wasaidizi wenu kukiuka maadili ya utumishi wa umma. Tambueni kuwa kwenye ngazi ya mikoa na halmashauri ninyi ndiyo wasimamizi wa rasilimali fedha, watu na mali za wizara.

"Baadhi yenu mpo ambao mmechukua hatua pale mnapobaini mapungufu ya wale mnaowaongoza, wengine mpo kimya na mnaacha mambo yajiendee kiholela. Kuanzia sasa, endapo tutafanya kazi zenu, na mmekuwa mkitufanya tufanye kazi ambazo mlipaswa kufanya, tambueni kuwa mnatupa mashaka ya namna mnavyotosha kwenye hizo nafasi, kwenye hili nalo Katibu Mkuu anza kuchukua hatua haraka,"amesisitiza Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Awali, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema,majukumu ya msingi wizara ni upangaji ardhi, upimaji, umilikishaji, uthamini, usajili wa milki, ukusanyaji maduhuli yanayotokana na ardhi, usimamizi wa milki kuu,utatuzi wa migogoro kiutawala na au kupitia Mbaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.
"Aidha, ninatambua kuwa majukumu haya yote yamewekewa malengo ya utekelezaji ambayo yanatumika kupima ufanisi ya mwelekeo wa huduma zinazotolewa kwa wananchi na wizara. Natambua nyote mnajua kwa nini wizara iliamua kuanzisha ofisi za Ardhi za Mikoa Machi, 2020 kutoka kwenye kanda nane zilizokuwepo kwenda ngazi ya mikoa mfumo ambao ulianza kutumika mwaka 2008.

"Lengo letu lilikuwa ni kusogeza huduma kwa wananchi, kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri, kurahisisha utatuzi wa kero na migogoro ya ardhi na kuimarisha mfumo wa usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya sekta. Bado nina imani lengo hilo ni la muhimu,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news