NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt.Angeline Mabula amewaagiza makamishna wa ardhi nchini kuhakikisha ujenzi wa vituo vya mafuta unazingatia taratibu za mipangomiji na uendelezaji wa miji kwani kwa sasa vituo hivyo vinajengwa kila sehemu bila udhibiti.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula ameyabainisha hayo leo Septemba 6,2022 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi cha makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa 26 nchini.
"Nyote mnatambua tunayo programu ya urasimishaji makazi ya miaka 10 ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 2013 na itakamilika mwaka 2023.
"Wakati tunatekeleza programu hiyo, tumeendelea kushuhudia ongezeko la ujenzi holela na hivyo kuathiri ukuaji endelevu wa miji yetu. Mathalani, vituo vya mafuta hivi sasa vinajengwa kila sehemu bila udhibiti na uratibu mbele ya macho yenu kama wasimamizi wa sekta katika mikoa yenu. Hatuwezi kuendelea hivyo bila kuchukua hatua.
"Hili naagiza likasimamiwe ipasavyo na kwa nguvu zote. Kwenye kila jambo ambalo nilitaka tuzungumze hii leo nimetoa maelekezo ya namna ya kushughulika nalo na ninaamini Katibu Mkuu utachukua hatua stahiki.
"Natambua Katibu Mkuu umefanyika uchambuzi wa kutosha kuhusu uwezo na udhaifu kwenye eneo la usimamzi na natambua tunaenda kuchukua hatua kuanzia leo,"amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, hafurahishwi kabisa na utendaji wa baadhi ya Makamishna Wasidizi wa mikoa hususani wale wa mikoa ya Rukwa na Simiyu.
"Hili haliwahusu ninyi pekee, nataka ujumbe uwafikie wataalamu wote wa sekta kuwa tutachukua hatua ili kuhakikisha tunaimarisha utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea. Tunao watumishi wengi wazuri,wekeni malengo na mkakati wa utekelezaji wake.
"Napenda kusisitiza kuwa, tutawapima kwa utendaji wenu na wale mnaowasimamia kwenye masuala yote kama tulivyowaelekeza. Upimaji wa utendaji kazi zenu utajikita kwenye masuala yote muhimu, lakini kwa umahsusi wake, tutawaoina sana kwenye maeneo ya utatuzi wa migogoro, makusanyo ya maduhuli na usimamizi wa raslimali watu (weledi wao, utendaji wao na uwajibikaji),"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.
Aidha, kwenye suala la usimamizi wa raslimali watu,Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, "tunahitaji kuliwekea utaratibu wa usimamizi ulio mzuri ili lisiwe chanzo cha kuzalisha migogoro. Ninalisema hili nikiwa natambua kuwa Kamati uliyounda Katibu Mkuu kushughulikia migogoro katika Mkoa wa Dar es Salaam imebaini uwepo wa migogoro ambayo chanzo chake ni watumishi wetu wasio waadilifu.Tuanze na hao na wengine ambao tuna taarifa zao za ukiukaji wa maadili ya kazi.
"Kama nilivyosema awali, kikao hiki sikupenda tuongee yale ambayo mmezoea kusikia kila siku, hayo tumeongea sana, kikao hiki nilitaka kiwasaidie kufanya tafakari na kuakisi utendaji wenu ili kutimiza matarajio ya wizara ya kuwahudumia wananchi.
"Kwa wale ambao mnapenda kuona kwa vitendo, tuko thabiti na tutachukua hatua kwenye yote niliyosema.Hatuwatishi, lakini mtambue tutakapochukua hatua, mjue tulisema,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.