NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wote Serikalini kuweka mkakati wa kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye ukumbi wa Kuringe mjini Moshi.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la agizo ni kusisitiza utekelezwaji wa maono na dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya utulivu ili kuendelea kufikisha maendeleo katika kila eneo.
Amesema hayo leo Septemba 21, 2022 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yayofanyika katika ukumbi ya Kuringe, Moshi Kilimanjaro.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani, Septemba 21, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Hassan Babu.
“Hatuna budi kuitunza amani yetu kulingana na umuhimu wake kwani amani ni tunda la upendo, utulivu, mshikamano na maridhiano.”
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa katika kutafuta na kudumisha amani na usalama.
“Jukumu la kudumisha amani na kuilinda amani ni ajenda ya kidunia inayomgusa kila mmoja, ili kulinda ustawi wa vizazi vya leo na kesho.”
Pia, amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchukua hatua na tahadhari zote zinazohitajika ili kuendelea kudumisha amani nchini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Hassan Babu (katikati) na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi katika maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani mjini Moshi.
“Serikali ya Awamu ya Sita, inafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa kwa kuweka mikakati mbalimbali ya maendeleo inayolenga kutokomeza umaskini. Umaskini ni chanzo kikubwa cha migogoro sehemu nyingi duniani kwa sababu watu wanagombania kufaidika na rasilimali chache zilizopo.”
Ameongeza kuwa kila palipo na amani, shughuli za kiuchumi na kijamii hufanyika kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi kwa ujumla. “Niwasihi wananchi kuendelea kutunza na kuilinda tunu ya amani tuliyojaliwa hapa nchini”
“Ni lazima tuendelee kuilinda amani nchini kwetu, Watanzania tuendelee kudhibiti yeyote mwenye nia ya kuiharibu amani yetu. Jukumu la kuilinda amani hii ni agenda yetu sote, tuitekeleze.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea mfano wa njiwa mweupe kama ishara ya kuhamasisha amani duniani, katika maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani iliyofanyika kitaifa mjini Moshi, Septemba 21, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Hassan Babu na kulia ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Zlatan Milisic.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono ajenda mbalimbali za maendeleo nchini ili kuhakikisha umaskini haugawanyi jamii bali uwe chachu ya kutafuta njia bora ya kujinasua katika hali hiyo.
Naye, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania, Zlatan Milisic ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa kinara katika kudumisha amani katika nchi za Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.
Aidha, alitoa wito kwa jamii yote nchini kuacha kuchukulia mzaha suala la uwepo wa amani kwani yapo mahusiano ya karibu kati ya amani na maendeleo. “Jamii yenye amani inaweza kuweka mipango yake ya maendeleo vizuri na kuitekeleza kwa ajili ya shughuli za maendeleo”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema kuwa viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wataendelea kusimamia utunzaji wa amani tuliyonayo kwani ni tunu muhimu tuliyojaliwa nchini.
“Sisi viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro tutaendelea kushirikiana na taasisi zote zikiwemo za dini kwani uwepo wa amani ni msingi wa ustawi wa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla”.