NA MATHIAS CANAL-WEST
SERIKALI imesema kuwa wathibiti ubora wa elimu ni mboni ya serikali katika kusimamia na kuimarisha ubora wa elimu nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof.Adolf Mkenda ameyasema hayo leo Septemba 29, 2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na wadhibiti ubora wa kanda zote nchini.
Amewataka wathibiti ubora kote nchini kusimamia kwa weledi zaidi ubora wa elimu kwani wao ni moyo na injini ya elimu.

"Walimu wamerundikana maeneo ya mjini kuliko vijijini lakini katika maeneo yote hayo kuna watanzania wengi wanaohitaji elimu, kwa sasa jambo kubwa ambalo tunapambana nalo ni walimu wengi kutaka kuhama kutoka vijijini kwenda mjini,"amesisitiza Waziri Mkenda na kuongeza kuwa;

Amesema kuwa, Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu ambazo ni pamoja na vitendea kazi na ubora wa madarasa.
Waziri Mkenda amesema kuwa, wakati serikali inaendelea kufanya mageuzi ya elimu nchini ni vyema wathibiti hao wa ubora wa elimu kuhakikisha kuwa wanatoa maoni ya namna ya kuboresha vigezo na sifa za ubora wa elimu.

Kadhalika ametoa kibali kwa walimu wanaoomba kwenda kusoma ambapo ametaka wapewe ruhusa ili kuongeza sifa na weledi katika utendaji kazi wao kwa kufuata taratibu na sheria za utumishi wa umma.