Zoran Maki aibuka, Yanga na Simba SC hawakamatiki Kimataifa

NA GODFREY NNKO

SAHAU kuhusu utani na misimamo ya ushabiki,leo Septemba 10, 2022 imekuwa kati ya siku njema kwa Watanzania wote, baada ya Klabu ya Yanga na Simba kuiwakilisha Tanzania vema katika michuano ya Kimataifa.
Ni kupitia mitanange ambayo imepigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam na ile iliyopigwa katika dimba la Bingu jijini Lilongwe nchini Malawi.

Mambo yalikuwa hivi

Yanga SC ya jijini Dar es Salaam chini ya mwalimu mkuu, Nasreddine Nabi imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini ambayo ilikuwa mwenyeji wa mechi ya kwanza ya Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mtanange huo ambao ulionekana wa kukamiana ulianza kwa dakika 45 za kwanza, timu zote kwenda mapumziko zikiwa hazina bao hata moja.

Katika mtanange huo uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, shujaa wa Yanga SC alikuwa ni mshambuliaji wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fiston Kalala Mayele.

Mayele alifunga mabao matatu kati ya dakika ya 47, 84 na 87 na kutoa pasi ya bao lingine lililofungwa na kiungo Feisal Salum Abdallah (Fei Toto) dakika ya 54 ya kipindi cha pili.
Yanga SC ina faida ya mabao manne ya ugenini, hivyo kazi yao ni kushinda mchezo ujao ili kuongeza nafasi ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Aidha, timu hizo zitarudiana Septemba 17, 2022 ndani ya dimba hilo la Benjamin Mkapa na mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Al Hilal ya Sudan na St.George ya Ethiopia.

Simba yashinda

Wakati huo huo,Simba SC imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, Nyasa Big Bullets FC katika mtanange wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni kupitia mtanange ambao umepigwa katika dimba la Taifa la Bingu huko jijini Lilongwe nchini Malawi leo Septemba 10, 2022.

Kupitia mwalimu wa muda, Juma Mgunda wekundu hao walifanikiwa kutwaa alama tatu kwa mabao washambuliaji Mzambia, Moses Phiri kwa tik-tak dakika ya 28 na mzawa, John Bocco dakika ya 84.

Baada ya mtanange huo, timu hizo zitarudiana Septemba 18, 2022 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Aidha, mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Primiero do Agosto ya Angola na Red Arrows ya Zambia.

Hata hivyo,mwalimu huyo wa muda amewapongeza vijana wake kwa kuonesha umakini na kupambana hadi kupata matokeo mazuri.

“Ninafurahi kuona vijana wamepata matokeo na haukuwa mchezo rahisi ila wachezaji wamepambana na kupata ushindi bado kuna kazi kwenye mechi zijazo kimataifa tutafanyia kazi makosa yetu,"amesema Juma Mgunda.
Katika hatua nyingine, mwalimu aliyeondoka Simba SC kabla ya kukamilisha mkataba wake raia wa Serbia,Zoran Manojlovic amewapongeza vijana wachezaji wa Simba kwa ushindi huo.

Manojlovic alichukua mikoba ya Pablo Franco aliyetimuliwa klabuni hapo Mei 31, 2022 huku na yeye akiondolewa klabuni hapo Septemba 6, 2022 baada ya klabu kuonekana kufanya vibaya.

Kocha huyo raia wa Serbia alikuwa kwenye taaluma ya kandanda kwa muda katika soka la Afrika ambapo klabu kama Wydad, Al Hilal ya Sudan ni moja ya timu ambazo aliwahi kuzinoa.

Manojlovic alipewa mkataba wa mwaka mmoja kuinoa timu hiyo ambapo Pablo alifutwa kazi ndani ya kikosi cha kutokana na kushindwa kufikia malengo ambayo alipewa ikiwa ni pamoja na kutwaa taji la Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la TFF na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya CAF wakati huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news